KOCHA PSG ATOA NENO KUHUSU UBINGWA

 | PARIS, Ufaransa     |

KOCHA Unai Emery ametoa neno kuhusu ubingwa wa Ligue 1 ambao Paris Saint-Germain ilifanikiwa kuutwaa juzi, akisema kuwa klabu hiyo itazidi kuchanua licha ya kukosa mafanikio katika michuano ya Ligi ya Mabingwa ikiwa naye ama hata akiondoka.

Juzi PSG iliiadhibu Monaco kwa mabao 7-1 na hivyo kutawazwa kwa mara ya tano ndani ya misimu sita na huku ikiwavua mabingwa hao watetezi.

Huku ikiwa imeshatwaa taji la Coupe de la Ligue, PSG inaweza kutwaa mataji matatu ya ligi za ndani endapo itanyakua la Coupe de France, lakini ufalme huo unaonekana bado hauwezi kulinda kibarua cha Emery.

Emery alikabidhiwa mikoba ya timu hiyo mwanzoni mwa msimu uliopita kutokana na umahiri wake kupenya katika hatua ya mtoano wa michuano hiyo ya Ulaya, lakini akajikuta akitupwa nje katika hatua ya 16 bora.

Kutokana na matokeo hayo, inaonekana wazi huenda ikashuhudiwa mkataba wake ambao unamalizika mwishoni mwa msimu huu, hauongezwi tena huku kukiwapo taarifa kwamba Thomas Tuchel, ndiye atakyepewa mikoba yake.

“Wakati nilipofanya utafiti wangu niliona kwamba ili uweze kuimarika Ulaya ni lazima kwanza ufanye hivyo katika kutwaa ubingwa wa Ufaransa,”     alisema kocha huyo mara baada ya ushindi huo wa juzi.

“Ukiangalia katika Ligi ya Ufaransa kuna timu kama Saint-Etienne ambao wametwaa ubingwa mara 10, Marseille mara tisa, Monaco na Nantes mara nane. Na leo tumefanikiwa kutwaa wa kwetu mara saba. Jambo hili litafungua nafasi nyingine katika mashindano mengine,”     aliongeza kocha huyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*