Kocha Ndanda: Simba mtatusamehe

NA ZAITUNI KIBWANA

KOCHA wa timu ya Ndanda, Khalid Adam, amesema hawatakubali kupoteza pointi kwa Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa kesho kutwa kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na BINGWA jana, Adam alisema anaiheshimu Simba lakini watawasamehe kwani hawatakubali kupoteza mchezo huo.

Adam alisema wanaendelea na maandalizi ili kuhakikisha wanapata pointi tatu ambazo zitawaweka katika mazingira bora zaidi katika msimamo wa ligi hiyo.

 “Simba tunaiheshimu ila hatuwahofii, sisi tunaingia kukabiliana nao kivyovyote vile ili mradi tuibuke na pointi tatu muhimu,” alisema.

Alisema kikosi chake kina majeruhi wawili ambao ni mshambuliaji, Vitalis Mayanga, anayesumbuliwa na nyonga na kiungo, Shaib Mnemba, aliyeumia kisigino.

Kocha huyo alisema wachezaji hao wanaendelea kufanya mazoezi maalumu ili waweze kuwa fiti na baadaye kuungana na wenzao.

Ndanda wako kwenye hatari ya kushuka daraja hivyo wanatakiwa kushinda michezo mitatu iliyosalia ili kujinusuru na kubaki Ligi Kuu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*