googleAds

Kocha Namungo alia Azam kumtesa

Mwandishi Wetu

KOCHA mkuu wa timu ya Namungo, Hitimana Thiery, amesema licha ya kufanya vizuri katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, mchezo uliomtesa zaidi msimu huu ni ile ya mzunguko wa kwanza dhidi ya Azam.

Katika mchezo huo Namungo walikubali kichapo cha mabao 2-1 katika  Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Lakini pia walivyorudiana mzunguko wa pili Namungo waliweza kutoka kifua mbele kwa ushindi wa bao 1-0 kwenye dimba la Majaliwa, Ruangwa, mkoani Lindi.

Akizungumza na BINGWA jana, Thiery alisema kipindi hicho walikuwa na wakati mgumu ukizingatia walikuwa wakihitaji pointi tatu muhimu ila hawakuweza kupata.

“Tulikuwa tukihitaji ushindi kwenye mchezo huo ila bahati haikuwa upande wetu kwani kila mbinu niliyojaribu waliweza kutuzidi na mwishoni wenzetu walishinda,” alisema Thiery.

Alisema pamoja na yote walivyorudiana katika Uwanja wao wa nyumbani waliweza kuwazidi na kupata ushindi katika mchezo huo.

Thiery alisema kwa sasa ameweza kukitengeneza vizuri kikosi chake ambacho wamekuwa wakipata matokeo hasa wanapocheza nyumbani kutokana na umakini waliokuwa nao.

Kwa sasa Namungo wanashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo kutokana na pointi 50, baada ya kucheza michezo 28 wakishinda mara 14, sare nane na kupoteza sita.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*