Kocha Al Ahly aahidi kuendeleza ubabe kwa Simba

TIMA SIKILO NA SALMA MPELI KOCHA wa Al Ahly, Martin Lasarte, ameahidi kuendeleza kichapo kwa wapinzani wao, Simba, katika mchezo wao wa marudiano Ligi ya Mabingwa Afrika, unaotarajiwa kuchezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Katika mchezo uliopita, Simba walikubali kichapo cha mabao 5-0, mechi iliyopigwa ugenini, nchini Misri. Akiuzungumzia mchezo huo, Lasarte alisema wanacheza ugenini lakini lengo ni kushinda kama ambavyo walishinda nyumbani. Alisema wao hawana uwanja wa nyumbani au ugenini, kote watakapokwenda wanachokifanya ni kutumia nafasi wanazozipata kufunga mabao. “Tumekuja Tanzania hatuwezi kuudharau huu mchezo na tunafahamu haitakuwa rahisi, kwani Simba si timu mbaya, hivyo tumejiandaa kukabiliana na hali yoyote, kama mchezo uliopita tulishinda kwa sasa hatuuhesabii akili yetu ipo kwenye mchezo wa kesho (leo),” alisema. Alisema kuna wachezaji wao wa kikosi cha kwanza ambao hawatacheza katika mchezo huo kutokana na sababu ambazo zipo nje ya uwezo, lakini hiyo haiwezi kuathiri kikosi chao. Aidha, alisema kuwa kubadilisha mazingira kwao kuna changamoto kubwa katika kila idara. “Tunashiriki katika ligi nyingi hata nyumbani na kila mchezo kwetu tunahitaji kuweka historia, tunahitaji pointi tatu ili tuweze kuendelea mbele,” alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*