KLOPP AIONYA REAL MADRID

LONDON, England    |  

KOCHA wa Liverpool, Jurgen Klopp, ameionya Real Madrid akisema kwamba, wasitarajie mteremko wakati watakapokutana nao katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Vinara hao wa Ligi Kuu England walikata tiketi hiyo usiku wa kuamkia jana kwa jumla ya mabao 7-6 dhidi ya AS Roma, licha ya kuambulia kipigo cha mabao 4-2 wakiwa ugenini katika Uwanja wa Stadio Olimpico.

Vinara hao bado wanakabiliwa na mtihani mgumu wakati Mei 26 mwaka huu wakapowavaa mabingwa hao watetezi, Real Madrid, ambao wametinga fainali kwa mara ya nne katika kipindi cha miaka mitano.

Hata hivyo, Klopp anasema kwamba, licha ya kuwa anafahamu vilivyo Real Madrid walivyokuwa na uzoefu, lakini anavyoamini siku hiyo watakuwa kwenye ubora wa hali ya juu.

“Kutinga fainali ni jambo zuri sana.Nimewahi kufika hatua hiyo mara chache sana. Lakini kutwaa ubingwa ni jambo zuri zaidi na siku hiyo tutakuwa tayari kufanya hivyo,” alisema kocha huyo.

“Sisi siyo wazoefu sana katika mashindano haya kuliko Real Madrid. Nadhani watu wote wanaipa nafasi kwa asilimia 80 timu ambayo imecheza mara nne fainali ndani ya miaka mitano, ila bado tutakuwa na nguvu za kuwakabili,” aliongeza kocha huyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*