googleAds

KLABU ZITUNZE KUMBUKUMBU ZA WACHEZAJI

SIMBA imenusurika kuondolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (FA), baada ya Polisi Dar es Salaam kuwasilisha rufaa kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wakipinga kumchezesha beki wa timu hiyo, Novat Lufunga, katika mchezo uliochezwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Uhuru.

Polisi Dar es Salaam walichukua uamuzi huo, baada ya kufungwa mabao 2-0, lakini wakiwa na ushahidi kuhusu rufaa yao kwamba, Lufunga alikuwa na adhabu ya kutumikia kadi nyekundu.

Rufaa iliyowasilishwa kwa shirikisho hilo, walieleza kwamba Lufunga alionyeshwa kadi nyekundu wakati  Simba ilipocheza na Coastal Union katika mchezo wa robo fainali uliochezwa mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na kufungwa mabao 2-0.

Kutokana na kanuni zinazotumika katika mashindano hayo kuwa wazi, ndicho kilichowasukuma viongozi wa Polisi Dar es Salaam kutumia udhaifu huo kuikatia Simba rufaa kwa kuwa waliona wamekiuka.

Polisi walikuwa na uhakika kwamba, Simba hawakustahili kumchezesha Lufunga kwa sababu hiyo iliyotajwa, kwani walitakiwa kuwa na kumbukumbu na wachezaji wao.

Hata hivyo, tunaliona tatizo la klabu kukosa kumbukumbu sahihi kuhusu wachezaji wao wanaopata kadi katika mechi mbalimbali za Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano mengine limekuwa ni kubwa.

Klabu nyingi zimekuwa na upungufu wa kuweka kumbukumbu za wachezaji wao, kwani Yanga waliwahi kupokwa pointi baada ya kumchezesha, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union, lakini pia Azam kitu ambacho kimekuwa kikiigharimu timu pale inapogundulika kuwachezesha wachezaji kimakosa.

Jukumu la kutunza kumbukumbu liko chini ya meneja wa timu kwani anatakiwa kuwa mwepesi wa kufuatilia kwa mwamuzi au kwa TFF na Bodi ya Ligi kadi wanazopewa wachezaji wao baada ya kumalizika kwa mchezo husika.

Tunaamini kwamba, kama mameneja watakuwa makini na kumbukumbu za wachezaji wao, hakika hilo lililotaka kutokea kwa Simba linaweza kuepukika.

Tunashauri kwamba viongozi wa klabu, waamuzi, TFF na Bodi ya Ligi washirikiane kujulishana kuhusu wachezaji wanaotakiwa kutocheza kutokana na kutumikia adhabu ili kuondoa usumbufu kama uliojitokeza kwa Polisi Dar es Salaam kufikia kuikatia Simba rufaa.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*