KIWANGO REAL MADRID HAKISOMEKI, MODRIC ANENA

MADRID, Hispania


 

TIMU ya Real Madrid imeendelea kupata matokeo yasiyoridhisha, baada ya kupoteza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya waliocheza usiku wa kuamkia jana kwa bao 1-0 dhidi ya CSKA Moscow.

Mabingwa watetezi hao wa michuano hiyo walio chini ya kocha Julen Lopetegui, walikubali kichapo hicho kutoka kwa vigogo hao wa Urusi, bao lililofungwa na mshambuliaji aliye kwa mkopo CSKA, Nikola Vlasic.

Vlasic alitikisa nyavu za Madrid mapema kabisa katika sekunde ya 65, bao lililodumu hadi mwisho wa mchezo huo na kuipa timu yake ya CSKA ushindi muhimu katika Kundi G.

Wakiondoka ugenini huko bila kutikisa nyavu za CSKA, Madrid walifikisha mechi ya tatu mfululizo bila kufunga bao, ikiwa ni rekodi mbovu kuwahi kutokea katika klabu hiyo kwa zaidi ya miaka 11.

Kichapo hicho kilifuatia baada ya Madrid kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Espanyol kwenye Ligi Kuu Hispania, kipondo cha mabao 3-0 kutoka kwa Sevilla na kulazimishwa suluhu na ndugu zao, Atletico Madrid wikiendi iliyopita.

Ikumbukwe kuwa, Madrid walianza vyema michuano hiyo kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Roma, lakini juzi waligonga mwamba kwa Warusi hao na kuzidisha presha kwa kocha wao huyo, Lopetegui.

Katika mtanange huo, Madrid waliendelea kuonesha jinsi gani walivyo na safu butu ya ushambuliaji, kwani walishindwa kabisa kufunga bao, licha ya kupiga mashuti 26 langoni mwa CSKA.

Takwimu zinaonesha kuwa, hiyo ni idadi kubwa ya mashuti yaliyopigwa na Madrid bila kupata bao katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, tangu mtandao wa kukusanya ‘data’ wa Opta ulipoanza kushughulika na mambo hayo msimu wa 2003-04.

Mashuti ya nyota wa Madrid, Casemiro, Karim Benzema na Mariano, yote yaligonga mwamba, huku mlinda mlango wa CSKA, Igor Akinfeev, yeye hakupata tabu sana, kwani ni mashuti manne tu ya Madrid ambayo yalimlenga katika mchezo huo.

Kiwango hicho cha kusikitisha cha Madrid kimeibua mijadala kuwa hilo ni janga kubwa kwa wakali hao wa Hispania, lakini kiungo wa timu hiyo, Luka Modric amekanusha suala hilo.

Modrid alisema Real Madrid bado ipo vizuri, licha ya kupoteza dhidi ya CSKA.

“Hakuna janga baya kwetu, suala hapa ni kwamba hatujacheza katika kiwango chetu ambacho tunatakiwa kukionesha uwanjani,” alisema Modric, ambaye katika mchezo huo wa juzi alianzia benchi.

“Naamini, bila shaka yoyote, tutarejea kwenye hali ya ushindi. Niwapongeze CSKA kwa jinsi walivyojipanga vyema, wana timu yenye wachezaji wazuri. Walitumia vyema nafasi walizozipata, lakini sisi hatukuzitumia,” aliongeza.

Madrid wanatarajia kukutana na shughuli nyingine nzito wikiendi hii, watakapokutana na Deportivo Alaves katika mchezo wa La Liga.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*