Kiwango Man Utd chamtia hofu Pogba

LONDON, England

STAA Paul Pogba amekiri akisema kwamba timu ya Manchester United juzi ilicheza kwa kiwango cha chini dhidi ya West Ham na akasema kuwa ni lazima waimarike zaidi endapo wanataka kuifunga Barcelona katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, itakayopigwa kesho katika Uwanja wa Camp Nou.

Katika mchezo huo, Man United waliweza kupata ushindi wa mabao 2-1 wakiwa nyumbani katika Uwanja wao wa Old Trafford, yaliyofungwa na kiungo huyo, Pogba kwa njia ya penalti.

Bao la kusawazisha la West Ham lilifungwa na Felipe Anderson, lakini timu hiyo ingeweza kuongoza kwa mpira uliogonga mwamba na makosa ya mlinda mlango, David de Gea kushindwa kuzuia mpira uliopigwa na Michail Antonio na kwenda kimiani, lakini bao hilo likakataliwa.

Wageni hao pia wasingeweza kuondoka mikono mitupu, lakini nyota wao, Ryan Fredericks akawaangusha, baada ya kumfanyia madhambi  Anthony Martial  ndani ya eneo la hatari na hivyo kumpa nafasi Pogba kufunga bao la ushindi dakika ya 80.

Matokeo hayo yamekifanya kikosi hicho cha  Ole Gunnar Solskjaer kubakiza pointi mbili dhidi ya timu inayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, Chelsea na yamewaweka sawa, wakati kesho watakapokuwa katika Uwanja wa Camp Nou wakitafuta kulipiza kisasi cha kufungwa bao 1-0  katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

“Hatukucheza kwa kiwango kizuri, ingawa tumepata matokeo haya,” Pogba alikiambia kituo cha televisheni cha BT Sport.

“Mechi ilikuwa wazi, lakini hatukucheza vizuri. Kwa nafasi na pasi tulizozipiga ni wazi tulicheza kwa kiwango cha chini na hawakuwa tishio,” aliongeza staa huyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*