googleAds

KISA CHA YAMOTO BAND KUVUNJIKA KIMYA KIMYA-4 Marombosso afunguka

 

NA TIMA SIKILO

WASANII wa Yamoto Band wamekuwa wakijitetea na kusisitiza kwamba kundi lao halijavunjika na bado wako pamoja, lakini kuna dalili za wazi zinaonyesha kwamba Yamoto Band imevunjika kimya kimya na ndiyo maana kila mmoja ameendelea kutoa kazi zake binafsi.

Mpaka sasa waimbaji wa bendi hiyo kama Enock Bella na Bela Flavor wameshatoa nyimbo zao kila mmoja, huku Aslay akionekana kutoa hasira zake zaidi kwa kutoa nyimbo nyingi zaidi ya wenzake ambapo hadi sasa amekwishaachia takribani 10.

 

Ilipoishia wiki iliyopita…

Mbaya zaidi aliamua kuhama, lakini jinsi alivyohama ilikuwa kama kwa shari fulani hivi, kwani tumeshtukia mtu anakuja bila taarifa na baunsa, ambaye tulikuwa tunamtumia kwenye bendi yetu ya Yamoto na baadhi ya washkaji wetu, ila ujio wao ulikuwa wa shari, kwani walishindwa hata kusalimia, wakaanza kuhamisha vitu na hapo ndipo ilikuwa mazima mpaka leo. Hivyo ikiwa anataka kujua kitu anachofanya ni kupiga simu basi hakuna mazungumzo mengine.

 

Endelea…

Baada ya Beka Fleva kusema kwamba Yamoto haijakufa, naye Enock aliulizwa swali kuhusiana na hatima ya kundi hilo, hasa kwa upande wa viongozi, kutokana na mambo yaliyotokea hadi kuwaruhusu wasanii hao kufanya kazi binafsi kila mmoja.

Enock anasema Yamoto Band haijakufa na ukweli ni ngumu sana kusimama na kuwaambia mashabiki kuwa Yamoto imekufa, kwani kauli hiyo inaweza kusababisha kila mmoja wetu akapoteza mashabiki na hata kuchukiwa kabisa na wanaoipenda bendi hiyo.

Ukweli ni kwamba Yamoto Band haiwezi kukamilika ikiwa na mtu mmoja au watatu, inahitaji wote wane, ili iwe Yamoto Band, ila Yamoto ipo na itakapotokea kuna kazi ya kundi basi tutafanya na hata ikitokea mtu anapata shoo ya pamoja, huku akiwa na shoo yake binafsi, basi mtu ataangalia maslahi yako wapi atajua mwenyewe cha kufanya.

Naye Marombosso, ambaye ameonekana kwa kiasi fulani ndio chanzo cha Yamoto kufikia ilipofikia sasa, amefunguka kuwa bendi haijakufa, lakini alikiri kwamba mtindo waliouanzisha wa kila mtu kufanya kazi zake binafsi ni wazi kwamba kundi linaweza kufa.

Marombosso anasema sababu kubwa ya kuonekana kuwa kundi limekufa ni kukaa kimya kwa muda mrefu bila kutoa kazi za kundi na waimbaji wa kundi hilo kuendelea kutoa kazi binafsi.

Msanii huyo, ambaye mpaka sasa ndiye pekee ambaye hajatoa wimbo binafsi tangu Yamoto Band iparaganyike, anakiri kwamba ni kweli mfarakano ulitokea kati yake na Aslay, ila halikuwa tatizo kubwa, kwasababu hakuwa amekosana na mtu.

“Mimi sikuona kama lilikuwa ni tatizo kubwa kwa kuwa sikukosana na mtu, ila nilikuwa nimejaribu kuzungumza na shemeji kumwelewesha ukweli  juu ya kile alichokuwa ananikosea,” anasema Marombosso, akirudia maelezo ya Enock Bella, ambaye alisema shemeji yao (mzazi mwenzake na Aslay) alikuwa akitoa siri za uhusiano wa nje za msanii huyo kwa mpenzi wake.

Marombosso, ambaye ameonekana kwenye wimbo wa Wasafi (WCB) uitwao Zilipendwa bila ya kuwa na maelezo kama ameshirikishwa na kuonyesha kuwa ni msanii wa ‘lebo’ hiyo, lakini hakujakuwa na taarifa yoyote ya kutambulishwa rasmi kama ni mmoja wa wasanii wanaomilikiwa na Diamond, amesema kwamba yeye na Aslay huwa wanaongea, ingawa si kama zamani, ingawa si kwa ukaribu kama ilivyokuwa zamani.

Sehemu inayofuata itaelezea sababu nyingine ambazo zinahusishwa za kishirikina, ikidawa kuwa ndio chanzo cha Yamoto kuvunjika kimya kimya, ingawa hadi sasa sababu kubwa inaonekana ni mke wa Aslay kuwa chanzo cha kuivunja Yamoto kwa maelezo ya wasanii hao. Itaendelea…

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*