googleAds

Kipenzi cha Mo mtegoni Simba

NA MWANDISHI WETU

NDANI ya kikosi cha Simba, kuna wachezaji wanaotajwa kuwa vipenzi vya Mwenyekiti wa Bosi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’, akiwamo Jonas Mkude.

Japo mfanyabiashara huyo bilionea amekuwa akijificha juu ya hilo kwa kuonyesha mapenzi kwa wachezaji wote wa Simba, wakiwamo mashabiki, lakini mwisho wa siku, unaambiwa kuna ‘washkaji’ wake ambao hutamani kuwaona wakicheza kila mechi.

Hata hivyo, kama wanavyosema waswahili, ‘upele unawapata wasio na makucha’, ndivyo ilivyo kwa Mo Dewji dhidi ya wachezaji anaowazimia kwani wamekuwa hawamtendei haki kwa kumfurahisha mara chache chache mno.

Wakati Mkude angalau akiwa anaifanya kazi yake ipasavyo awapo uwanjani, lakini yupo kijana kutoka maeneo ya Tabata Savanna, Dar es Salaam ambaye naye anatajwa kuwa kipenzi cha Mo, lakini akishindwa kumfurahisha bosi wake huyo.

Mchezaji huyo si mwingine, bali ni Ibrahim Ajib ‘Mzee wa Makorokocho’, mwenye uwezo wa hali ya juu wa kusakata kabumbu.

Ajib ambaye aliyerea Simba msimu uliopita akitokea Yanga, kwa sasa anaonekana wazi kupoteza imani yake kwa Wanamsimbazi ambao ni ‘juzi’ tu walikuwa wakitembea vifua mbele wakijivunia kumng’oa nyota huyo kutoka Jangwani.

Mkali huyo wa asisti, kwa sasa hana nafasi katika kikosi cha Simba chini ya Kocha Sven Vandenbroeck na msaidizi wake, Seleman Matola ambao wanafanya kazi kwa ushirikiano wa hali ya juu, wakipewa sapoti na Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu. 

Chanzo chetu kutoka ndani ya Simba, kimesema: “Yaani kati ya wachezaji ambao wanachezea bahati ni Ajib, pamoja na kupendwa na mshua (Mo Dewji), lakini ameshaanza kupoteza umaarufu wake ndani ya timu.

“Huwezi kuamini kwa sasa hayupo hata kwenye 20 ya mwalimu, hapo unategemea nini? Tusubiri tu, lolote linaweza kutokea mwishoni mwa msimu na hakuna atakayemtetea maana kila mtu anataka kuona timu ikipata mafanikio, kama huna msaada na timu, hakuna atakayekuwa na habari na wewe.”

Alisema ili Ajib areejsha imani kwa mashabiki wa Simba, viongozi na hata bodi ya wakurugenzi, anatakiwa kujitafakari na zaidi kujifua vilivyo kurejesha makali yake, hasa kipindi hiki ligi ikiwa imesimama.

Tayari uongozi wa Simba, umeweka wazi kupanga kukiboresha zaidi kikosi chao kwa kusajili wachezaji wa kiwango cha juu na kuachana na wale wasio na msaada na timu hiyo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mbatha, ameliambia BINGWA kuwa lazima wakibomoe kikosi chao baada ya kumalizika kwa msimu huu.

Alisema japo wachezaji wao wengi wapo vizuri, lakini wameona kuna umuhimu wa kuwachuja baada ya kupokea ripoti ya kocha wao mwishoni mwa msimu.

“Tutajua nini kinahitajika baada ya mwalimu kukabidhi ripoti yake mwishoni mwa msimu, lakini mkakati wetu ni kubakiwa na wachezaji wenye uwezo wa kutufikisha pale tunapotarajia, hasa mafanikio ya anga ya kimataifa,” alisema Senzo.

Pamoja na hayo, Simba ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kutokana na pengo kubwa la pointi walizonazo dhidi ya wanaowafuatia, Azam na Yanga.

Hadi ligi hiyo inasimamishwa kutokana na hofu ya kuenea kwa virusi vya Corona, Simba ipo kileleni ikiwa na pointi 71 baada ya kucheza mechi 28, wakati Azam ina pointi 51, ikishuka dimbani mara 28 na Yanga iliyokipiga mechi 26, ikiwa na alama 50.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*