KINACHOMPA JEURI ZAHERA KUELEKEA ‘KARIAKOO DERBY’


NA WINFRIDA MTOI


 

HOMA ya pambano ya Simba na Yanga, linalotarajiwa kupigwa mwishoni mwa wiki hii, imezidi kupanda kwa mashabiki na wadau wa timu zote kila mmoja akiwaza atatokaje.

Ni kawaida inapokaribia mechi hiyo mawazo ya wadau wengi wa soka nchini huelekeza akili katika mchezo huo, huku baadhi ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara ikiahirishwa.

Katika kudhihirisha hilo, tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetangaza kuahirishwa kwa mechi zote zilizopangwa kuchezwa Septemba 26, 27 hadi pale mtanange huo utakapomalizika.

Lengo la kufanya hivyo ni kutaka kutoa muda wa kutosha kwa timu hizo kufanya maandalizi kwa vikosi vyao na mara nyingi hutoka nje ya Jiji la Dar es Salaam.

Pia, hata mwamuzi wa mchezo huo, huwa ni gumzo na kila mmoja akitaka kufahamu nani anaweza kubeba jukumu hilo zito ambalo   huambatana na mzigo wa lawama.

Ukiachana na hayo, mzigo mzito wa lawama katika mechi za ‘derby’, mara nyingi huwaangukia zaidi makocha ambao wanafikia hatua ya kutofahamu hatima ya vibarua vyao baada ya mchezo huo.

Imeshuhudiwa baadhi ya makocha waliozinoa  Simba na Yanga wakipata changamoto na hata  vibarua vyao kukatishwa baada ya mchezo  wa kuzikutanisha timu hizo kutokana na matokeo  yanayopatikana.

Hali hiyo huwafanya makocha wengi kuwa na presha na mchezo huo, kwa sababu wanajua kuwa pona yao itatokana na matokeo yatakayowaridhisha viongozi na mashabiki.

Presha kubwa inakuwa kwa makocha, kwasababu endapo siku ya mchezo huo kikosi kitaonekana tofauti na kushindwa kupata matokeo yaliyotarajiwa, lawama zote huangukia kwa kocha hata kama makosa yamefanywa na wachezaji.

Ukiangalia katika mechi za ligi hiyo zilizochezwa hadi sasa, Yanga haijapoteza hata moja, baada ya kushinda zote nne kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Mkongomani, Mwinyi Zahera, tangu amefika katika ardhi ya Tanzania mwanzoni mwa mwaka huu, alianza kukaa katika benchi la Yanga uwanjani wakati wa mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rayon Sports.

Licha ya kushinda mechi zote za ligi, mashabiki wa Yanga bado wanaonekana kutokiamini kikosi chao, huku wakiwa hawajaelewa vizuri falsafa za Zahera, ambaye anaonekana kuwa na misimamo yake.

Hivi karibuni mashabiki wa Yanga walionekana kukerwa na kitendo cha kocha huyo kumpa nafasi kipa Mkongomani, Claus Kindoki katika mchezo na Stand United, walioshindwa kwa mabao 4-3, wakidai mlinda mlango huyo hakuwa mzuri kama Benno Kakolanya, hivyo kuwa na wasiwasi kwamba anaweza kupangwa katika pambano la watani.

Zahera alitua Yanga, akiwa ni kocha ambaye hakupewa uzito mkubwa na mashabiki wa timu hiyo, kutokana na wasifu (CV) wake kutokuwa mkubwa sana, japo ni kocha msaidizi wa kikosi cha Taifa cha DR Congo.

Kocha huyo mwenye uraia wa Ufaransa, anaonekana amefundisha timu mbalimbali ndani na nje ya DRC, lakini amekuwa hakai kwa muda mrefu.

Ukiachana na timu ya Taifa aliyopo hivi sasa kama kocha msaidizi, timu nyingine alizowahi kufundisha Zahera kabla ya Yanga ni DC Motema Pembe kwa mwaka mmoja tangu 2015-2016.

Mwaka 2010, alifundisha kikosi cha AFC Tubize ya Ubelgiji akiwa kocha mkuu, lakini aliondoka baada ya miezi kadhaa na kurejea tena mwaka 2014 na kuwa msaidizi.

Kocha huyo aliyetunukiwa Diploma na leseni A ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), ameifundisha pia timu ya SC Feignies ya Ufaransa kuanzia mwaka 2000 hadi 2010.

Msimamo wake kuelekea mechi ya Simba

Zahera ameweka wazi kuwa, hana presha yoyote ya mechi za derby, kwa sababu akiwa mchezaji amekutana nazo na pia kama kocha amewahi kukaa kwenye benchi, huku kukiwa na idadi kubwa ya mashabiki waliomzunguka.

“Wakati nikiwa mchezaji nilicheza mechi zenye presha ya mashabiki wengi Ubelgiji, mojawapo nikiwa Antwerp FC, tukacheza na Boom, Ufaransa ilikuwa Amiens dhidi ya Abbeville.

“Nikiwa kocha, nilisimama katika mechi ya timu ya Taifa ya DR Congo dhidi ya Congo Brazzaville CHAN mwaka 2015, tulikwenda mapumziko tukiwa tumefungwa 2-0, lakini ndani ya dakika 28, tukasawazisha na mwisho wa mechi tukaibuka na ushindi wa mabao 4-2 na uwanjani kulikuwa na mashabiki zaidi ya 100,000,” anasema Zahera.

Anaeleza kuwa, mechi nyingine ambayo ilikuwa na upinzani mkubwa alipokuwa Motema Pembe, walikutana na Vita Club na kushinda bao 1-0, mbele ya mashabiki 100, 000.

“Kipindi hicho ilikuwa nimetokea Ulaya, niliitwa timu ya Taifa ya Congo, lakini viongozi wa Motema Pembe waliniomba kwa muda kusimamia timu yao ambayo haijawafunga Vita Club kwa miaka saba.

“Hivyo kwa mechi tunayokutana na Simba haiwezi kunipa presha yoyote, kwasababu mimi ni kocha ninajua nini cha kufanya ninapoingia katika mchezo unaozikutanisha timu zenye upinzani,” anatamba Zahera.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*