Kim Poulsen, Brandts vitani Yanga

NA ZAINAB IDDY

HABARI ndiyo hiyo kwamba muda wowote Yanga itakuwa chini ya kocha mpya, huku majina kadhaa maarufu yakitajwa kurithi mikoba ya Mwinyi Zahera ambaye anaonekana kuanza kuchokwa Jangwani.

Baada ya kujizolea maujiko kutoka kwa wapenzi wa Yanga kutokana na kazi nzuri aliyoifanya msimu uliopita, akiwa na kikosi kilichoonekana kuwa cha kawaida, hatimaye Wanajangwani, wameanza kuchoshwa na mbinu za kocha huyo.

Mbali ya mbinu zake kuonekana kutofua dafu kwa wapinzani, hata katika mechi za nyumbani, lakini pia usajili unaodaiwa kufanywa na kocha huyo kwa wachezaji wa kigeni, nao umechangia fukuto la kutaka kufungashwa virago.

Baada ya ‘kuteseka’ msimu uliopita, wapenzi wa Yanga walibuni mpango wa kuichangia timu yao iweze kufanya usajili wa nguvu utakaowawezesha kuhimiri vishindo vya watani wao wa jadi, Simba.

Lakini mwisho wa siku, Wanajangwani hao waliambulia kupata wachezaji wa ‘kusubiriwa hadi wachanganye’ ambao leo hii wamewafanya mashabiki wa timu hiyo kutotamani kusikia stori za soka.

Hilo limekuja ikiwa ni baada ya kutofanya vizuri katika michuano ya kimataifa, ikikumbukwa juzi tu ilipochapwa mabao 2-1 na Pyramids ya Misri katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Na sasa wakiwa wanatarajia kuwafuata Pyramids kwao kuona kama wanaweza ‘kupindua meza’ kwa kushinda na kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo ya kimataifa, kuna majina yameanza kujadiliwa ili kubeba mikoba ya Zahera.

Baadhi ya majina hayo, wapo makocha waliowahi kuinoa Yanga kwa mafanikio makubwa ambao ni Raoul Shungu, Hans van der Pluijm, Ernie Brandts na aliyekuwa kocha wa timu ya Taifa, Kim Poulsen.

Taarifa ambazo BINGWA limezipata jana kutoka ndani ya Yanga, zinasema kuwa kati ya makocha hao, anayepewa nafasi kubwa ni Poulsen, japo wapo wanaompigia debe Pluijm kutokana na rekodi yake kwa Wanajangwani hao, akwia amewapa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara mbili.

“Suala la kumuondoa Zahera Yanga, lipo kwa muda mrefu, lakini mara kwa mara wanapotaka kuchukua maamuzi hayo, baadhi ya viongozi wa timu wamekuwa wakizuia kwa madai ya kumpa muda.

“Lakini kutokana na matokeo ya jana (juzi), aina ya timu ilivyochezwa na kauli za kocha anazozungumza, kunatoa nafasi mkubwa kwa uongozi kutimiza azma ya kumrejesha Pluijm au hata huyo Shungu,” kilisema chetu cha uhakika.

Juu ya Pluijm, mtoa habari wetu huyo aliongeza: “Kama Pluijm atakubali kurudi Tanzania kufanya kazi na Yanga, uongozi upo tayari kumtumia tiketi ili aje haraka aweze kuanza kazi baada ya mchezo wa marudiano dhidi ya Pyramids.”

Kuhusiana na Shungu, Poulsen na Brandts, mtoa habari wetu mwingine alisema: “Wapo makocha wengi wanaotaka kuifundisha Yanga, walianza kutuma maombi yao tangu msimu uliopita, japo kwa sasa idadi imeongezeka.

“Uongozi unachosubiri ni matokeo ya mechi dhidi ya Pyramids, hata kama tutapita na kutinga makundi, sidhani kama Zahera atabaki. Ukiachana na Hans (Pluijm) ambaye amekuwa akitajwa sana, kuna majina mapya yameingia ambayo yamebadili mtizamo wa watu.

“Mtu kama Shungu aliifanyia makubwa Yanga na kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati Uganda, lakini na Poulsen rekodi yake Taifa Stars inambeba, wengi wanamkubali. Na Grandts naye ana nafasi, sasa hapa ni suala la kusubiri kuona nani atachukua nafasi ya Zahera kama itaonekana inabidi atuachie timu yetu.”

BINGWA lilimtafuta Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela ili kuzungumzia hilo ambapo alisema kwa kuwa hawajatangaza kuachana na Zahera, hawezi kuzungumza juu ya kocha mpya.

“Wapi tumetoa taarifa rasmi tumeachana na Zahera? Nawezaje kuzungumzia suala ambalo halijatoka kwetu? Kwa ufupi, Zahera ni kocha wetu na uongozi kwa sasa upo katika kutafakari namna ya kwenda kupata ushindi Misri, sio hilo jambo.”

Kwa upande wake, Pluijm, ameliambia BINGWA kuwa hadi jana jioni, alikuwa hajazungumza na kiongozi yeyote kutoka Yanga japo tetesi hizo amezisikia.

“Sijazungumza na kiongozi yeyote kutoka Yanga, nitatoa msimamo wangu baada ya kupata hizo taarifa kutoka kwa wahusika, kwa sasa siwezi kusema jambo lolote.”

Iwapo kama Pluijm atarejea Yanga itakuwa ni mara ya tatu kuinoa timu hiyo ambayo aliwahi kuipa mafanikio kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili na kuifikisha hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*