KILIWAKA ARSENAL WANOGA, JIJI LA MADRID LAKOSA MBABE

LONDON, England

STRAIKA Danny Welbeck jana alikuwa mwiba mkali kwa mabeki wa Southampton, baada ya kuziona nyavu zao mara mbili na kuisaidia Arsenal kushinda mabao 3-2.

Huku ukiwa ni ushindi wa sita mfululizo katika michuano mbalimbali, matokeo hayo yamewafanya Gunners wafikishe pointi 54, wakihitaji 13 sasa kuwafikia Tottenham wanaoikamilisha ‘top four’.

Kikosi cha kwanza cha Arsene Wenger kilikuwa na mabadiliko makubwa, kwani hakikuwa na mastaa wake saba walioiua CSKA Moscow.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu England, Southampton walikuwa wa kwanza kuichokoza Arsenal kwa bao la Shane Long lililotokana na kutoelewana kati ya kipa Petr Cech na beki wake, Shkodran Mustafi.

Arsenal waliokuwa nyumbani walicharuka kwa bao la Pierre-Emerick Aubameyang, kabla ya Welbeck kuongeza jingine.

Charlie    Austin     aliisawazishia Southampton lakini Welbeck ambaye hakuwa amefunga katika ligi tangu Septemba, mwaka jana, aliihakikishia Arsenal pointi tatu.

Mtanange huo ulimshuhudia beki Jack Stephens akilimwa kadi nyekundu, majanga ambayo pia yalimkuta kiungo wa Arsenal, Mohamed Elneny.

Nao mabingwa watetezi wa La Liga, Real Madrid, jana walishindwa kuutumia vyema uwanja wao wa Santiago Bernabeu, baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Atletico Madrid.

Timu hizo zenye viwango vya kuridhisha katika wiki za hivi karibuni, zilikutana tena jana baada ya kupita miezi mitano tangu walivyotoka suluhu kwenye mechi yao ya awali ya La Liga.

Mchezo huo ulitarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua kutokana na vita kali baina ya timu hizo zinazowania kumaliza msimu kwenye nafasi ya pili ambayo kabla ya mechi hiyo ya jana ilikuwa inashikiliwa na Atletico.

Kipindi cha kwanza cha mchezo huo kilikuwa ni kigumu kwa pande zote mbili, zilizokwenda mapumziko bila kutikisa nyavu, lakini kipindi cha pili Madrid walirudi na kasi na baada ya dakika nane tu, Cristiano Ronaldo aliipa timu yake hiyo bao la kuongoza.

Staa huyo aliendeleza wimbi la kutupia, akifunga bao lake hilo la 50 ndani ya miezi 12 na kufikisha mabao 650 katika muda wote aliocheza soka.

Hata hivyo, Atletico hawakuonesha dalili ya kukata tamaa na dakika ya 57 katika kipindi hicho cha pili, straika Antoine Griezmann aliisawazishia timu yake akitumia pasi ya winga, Vitolo na hadi dakika 90 zinamalizika, timu hizo ziligawana pointi.

Kutokana na matokeo hayo, Atletico waliendelea kushikilia nafasi ya pili kwa pointi 68 nyuma ya vina ra Barcelona (79), Madrid nafasi ya tatu pointi 64.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*