kila mtu ashinde nyumbani kwake

SIMBA ‘NEVER DIE AT HOME’

NA HUSSEIN OMAR

SIMBA ‘Never Die At Home’, ndiyo, Wekundu wa Msimbazi hao hawajapoteza mchezo wowote wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kwenye ardhi yao ya nyumbani.

Ni kwa kufahamu hilo, Simba wametamba kuendeleza wimbi lao la ushindi watakapoikaribisha AS Vita ya DR Congo katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya michuano hiyo, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 jioni.

‘Do or Die’

Kutokana na jinsi walivyopania kushinda mchezo huo, Simba wamekuja na kaulimbiu ya ‘Do or Die’, ikimaanisha kuwa leo ni kufa au kupona watakapowavaa wageni wao hao, huku lengo lao kuu likiwa ni ushindi utakaowawezesha kutinga hatua ya robo fainali.

Kikosi cha Simba juzi na jana kilifanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Taifa, kujiandaa na mchezo huo wa kukata na shoka huku Kocha Mkuu wa Wekundu wa Msimbazi hao, Patrick Aussems, akiweka mkazo zaidi katika suala zima la kufunga mabao.

Katika hilo, Aussems raia wa Ubelgiji, anaamini kuwa hakuna cha kupoteza leo kama itakavyokuwa kwa AS Vita, hivyo njia pekee ya kuwawezesha kutinga robo fainali ni kushambulia kwa nguvu zote ili kuvuna mabao mengi na ndipo mengine yafuate.

Aussems alonga

Akizungumza na BINGWA juzi baada ya mazoezi ya kikosi chake yaliyofanyika Uwanja wa Taifa, Aussems alisema ukakika wa kushinda ni mkubwa kutokana na maandalizi kabambe aliyoyafanya.

“Kwa upande wangu, nimemaliza kazi, kilichobaki ni wachezaji kufanya kile nilichowaelekeza. Kama unavyofahamu huu ni mchezo wetu wa mwisho, hivyo lazima tupigane kupata matokeo,’’ alisema Aussems.

Mbelgiji huyo alisema pamoja na mambo mengine, amewasisitizia vijana wake kuwa makini, hasa washambuliaji kuhakikisha hawapotezi nafasi yoyote wanayoweza kuipata, akifahamu ni mabao pekee yatakayoamua mshindi wa mchezo huo.

Kwa upande wa mabeki, amewataka kutocheka na washambuliaji wa AS Vita ambao wanaonekana kuwa na uchu wa mabao, wakifahamu hiyo ndiyo njia pekee inayoweza kuwavusha kwenda robo fainali ya michuano hiyo.

Kikosi

Kwa upande wa kikosi, Aussems huenda akapanga kikosi chake kama ifuatavyo; kipa Aishi Manula, beki wa kulia ni Zana Coulibaly, kushoto ni Asante Kwasi, mabeki wa kati ni Erasto Nyoni na Pascal Wawa, wakati viungo ni James Kotei, Hassan Dilunga na Clatous Chama.

Watakaoongoza safu ya ushambuliaji ni nahodha, John Bocco, akisaidiana na mkali wa kucheka na nyavu, Meddie Kagere pamoja na Emmanuel Okwi.

Lakini katika benchi, kunatarajiwa kuwapo kipa Deogratius Munish ‘Dida’, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Nicholaus Gyan, Muzamir Yassin, Paul Bukaba, Juma Rashid, Adam Salamba na Haruna Niyonzima.

Mo Dewji anasemaje?

Saa chache kabla ya vijana wa Wekundu wa Msimbazi kushuka uwanjani, mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed Dewji  ‘Mo Dewji’, amewataka kuhakikisha wanapambana kwa nguvu zao zote kushinda mchezo huo.

“Ili kufikia malengo yetu ya kuchukua ubingwa wa Afrika na kuweka historia, ni lazima tushinde mchezo wetu wa leo nawatakia kila kheri na Mungu awape nguvu,’’ alisema Dewji.

Vipi kuhusu Erato Nyoni?

Kuelekea mchezo huo wa leo, Erasto Nyoni aliyerejea dimbani akitokea katika majeruhi, ameliambia BINGWA kuwa wana kila sababu ya kushinda kutokana na maandalizi waliyoyafanya, lakini pia jinsi walivyopania kuweka heshima.

“Tunaomba mashabiki waje kwa wingi kushinda mchezo wa leo kutatupa nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali hivyo ni lazima tucheze kwa kujitoa na kufuata maelekezo yote tuliyopewa na benchi la ufundi,’’ alisema Nyoni.

Mashabiki waangalie mechi kwenye runinga zao?

Katika mchezo huo, mashabiki wa Simba wametakiwa kufika kwa wingi uwanjani kuwapa sapoti wachezaji wao badala ya kukaa nyumbani na kuutazama katika runinga zao.

Nyoni amewataka mashabiki hao kutokuwa na wasiwasi wowote wa matokeo leo, kwani kufika kwao kwa wingi wana imani kutawapa nguvu wachezaji katika kuipigania timu.

“Waje kwa wingi unajua mshabiki ni mchezaji wa 12 uwanjani, waje kutushangilia na sisi hatuwezi kuwaangusha kamwe,’’ alisema Nyoni.

Wachezaji wapigilia msumari

Wakifahamu jinsi mashabiki wao walivyokuwa na kiu ya kuiona timu yao ikitinga robo fainali ya michuano hiyo, wachezaji wa Simba kupitia nahodha wao, John Bocco, wameahidi kuwapa burudani wapenzi wote wa wakali hao wa Msimbazi hapa nchini na kwingineko.

“Tumejiandaa kushinda mchezo huo ili tuweze kuwapa raha mashabiki na viongozi wetu, tunaomba mashabiki waje kwa wingi kutupa sapoti, wao ndio mchezaji wa 12 uwanjani, tunaahidi hatutawaangusha,” alisema Bocco.

Simba inaburuza mkia katika Kundi D la michuano hiyo ikiwa na pointi sita, huku JS Saoura wakiongoza kwa pointi nane, Al Ahly ya Misri wakishika nafasi ya pili kutokana na pointi zao saba, sawa na AS Vita iliyopo nafasi ya tatu.

Kutokana na msimamo huo, timu itakayoshinda kati ya Simba na AS Vita, itaungana na mshindi baina ya Al Ahly na JS Saoura kutinga robo fainali kutoka kundi hilo.

Katika hatua nyingine, Mike Amine ambaye ni pacha wa kocha wa viungo wa Simba, Adel Zrane, ametua ndani ya kikosi hicho ili kuongeza nguvu.

Mike alionekana katika mazoezi ya Simba ya juzi Uwanja wa Taifa ambapo aliliambia BINGWA kuwa atakuwa na timu hiyo kwa wiki mbili kuwatibu majeruhi wa kikosi hicho na baada ya hapo, atarejea kwao Morocco.

“Nimekuja likizo na nitakuwa sehemu ya benchi la ufundi la Simba kwa muda wa wiki mbili, kama mambo yatakuwa mazuri, nadhani msimu ujao tutakwakuwa wote,’’ alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*