Kila la heri Taifa Stars, tupo nyuma yenu

MWANDISHI WETU

LEO timu ya Tanzania,Taifa Stars, itashuka kwenye Uwanja wa Taifa,Dar es Salaam kucheza na Guinea ya Ikweta ukiwa ni mchezo wa kwanza wa kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2021), itakayochezwa nchini Cameroon.

Taifa Stars inaanza kusaka tiketi nyingine ya AFCON  baada ya mwaka huu, kushindwa kufanya vizuri  katika michuano hiyo iliyofanyika nchini Misri na kuishia hatua ya makundi ikiwafungwa michezo yote.

Hivyo  basi mchezo wa leo tunautazama ni muhimu kwa Taifa Stars kushinda  katika uwanja wa nyumbani  ili kutengeneza mazingira mazuri ya kufuzu michuano hiyo,  huku tukiwa tumejifunza  kutoka kwa Lesotho iliyotupa changamoto  tulipohitaji kwenda Misri.

Tunakumbuka Taifa Stars ilifanya kosa la kutoka sare ya bao 1-1 na Lesotho katika mchezo wa kwanza wa kuwania kufuzu AFCON zilizopita uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, jambo ambalo tulikuja kujutia baadaye.

Kutokana na kupata sare kwa Lesotho,  ilituwia vigumu Taifa Stars kujihakikisha mapema kufuzu michuano hiyo, hali iliyotufanya kubiri matokeo ya mchezo mwisho kati ya Cape Verde na Lesotho ili tufuzu  hata kama tungeifunga Uganda kwa idadi ya mabao mengi katika mchezo wetu uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wachezaji wetu wa Taifa Stars watakuwa wanakumbuka matokeo ya Lesotho, hivyo wasirudie makosa katika mchezo wa leo, kinachohitaji ni mshindi wa pointi tatu na sio vinginevyo.

Tunaamini wachezaji wetu wanauwezo wa kuifunga Guinea ya Ikweta  kutokana na maandalizi mazuri yaliyofanyika, lakini tukiona wanacheza kwa kujituma zaidi kwa lengo la kulipigania taifa lao.

Kwa upande wetu, tunasema hakuna linaloshindika kwa Taifa Stars kuibuka na ushindi, ikizingatia watacheza mbele ya umati wa mashabiki wao ambao muda wote wa dakika 90 watakuwa wakiwapa hamasa ya kupata matokeo mazuri.

BINGWA  na Watanzania wengine kwa ujumla  tunaitakiwa Taifa Stars kila la heri katika mchezo wa leo ma matumaini yetu ni kuona wanaipeperusha vyema bendera yetu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*