Kikosi kimekamilika kuweka historia

NA ISIJI DOMINIC

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Emmanuel Amunike, yupo Maseru na wachezaji anaowaamini watafanya kile ambacho Watanzania wanakitaka Jumapili hii watakapowakabili wenyeji Lesotho, katika mchezo muhimu wa kufuzu Kombe la Afrika mwakani.

Taifa Stars na Lesotho wapo Kundi L pamoja na Uganda Cranes na Cape Verde. Mataifa mawili tu kutoka kundi hilo ndiyo yatakayoungana na mengine 22 kwa ajili ya michuano hiyo yenye hadhi kubwa barani Afrika iliyopangwa kufanyika Cameroon.

Amunike na vijana wake ambao ni tumaini la Watanzania, wameweka kambi ya takribani siku 10 nchini Afrika Kusini kunoa makali. Tofauti na maandalizi ya mechi dhidi ya Cape Verde ambapo wachezaji walivunja kambi ili kuzitumikia klabu zao kisha kurudi tena huku wengine wakipata majeraha, safari hii Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilipangua ratiba ya Ligi Kuu Bara ili kocha awe na muda wa kutosha na wachezaji wake.

Maandalizi ya Taifa Stars kuelekea pambano lao muhimu dhidi ya Lesotho yalipigwa jeki na Rais Dk. John Magufuli, aliyechangia Sh milioni 50 na kufungua milango kwa wadau wengine kujitokeza kuisapoti timu ya taifa.

Pigo kwa Taifa Stars ni kukosekana kwa Nahodha Mbwana Samatta, anayetumikia adhabu ya kukosa mechi moja na Frank Domayo ambaye anauguza majeraha. Hata hivyo, wachezaji ambao wanasafiri kwenda Maseru ni wazoefu na kocha Amunike alitumia muda wake kuchagua wachezaji wanaoendana na mfumo anaoutaka yeye.

Amunike amewajumuisha kikosini makipa Aishi Manula wa Simba, Beno Kakolanya wa Yanga na Benedictor Tinocco wa Mtibwa Sugar. Licha ya makipa wote kuwa na uzoefu wa Ligi Kuu Bara, Kakolanya alicheza mechi za mwisho mwisho hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika, wakati Manula na Tinocco wanatazamiwa kuzifikisha mbali timu zao katika michuano ya kimataifa ngazi ya klabu msimu huu.

Kwa upande wa mabeki, yupo Hassan Ramadhani Kessy, ambaye hivi karibuni alicheza dakika zote 90 na kuisaidia timu yake ya Nkana FC ya Zambia kutwaa ubingwa wa Kombe la Barclays. Beki mwingine anayecheza nje ya nchi ambaye anazidi kuimarika siku hadi siku ni Abdi Banda, anayekipiga Baroka FC ya Afrika Kusini.

Huwezi kuacha kutaja safu bora ya wachezaji mabeki nchini bila kuwamo Shomari Kapombe na Erasto Nyoni wa Simba, Kelvin Yondan na Gadiel Michael wa Yanga, Aggrey Morris na Abdallah Kheri wa Azam FC na Ally ‘Sonso’ Abdulkarim wa Lipuli FC, ambaye kiwango chake msimu huu kimemshawishi Amunike.

Viungo bora kwa sasa nchini ambao Amunike hakutaka kuwaacha katika safari ya Maseru ni Himid Mao wa Petrojet ya Misri, Simon Msuva anayekipiga Morocco akiwa na timu ya Difaa El-Jadidi, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Mudathir Yahya wote wa Azam FC pamoja na Salum Kimenya wa Tanzania Prisons.

Wamo pia kwenye kikosi cha Amunike viungo Feisal Salum aka Fei Toto wa Yanga na nyota wa Simba, Jonas Mkude na Shiza Kichuya, ambao wana uwezo wa kubadili mchezo muda wowote na pia kuchezesha timu.

Idara ya ushambuliaji japo itamkosa Samatta, lakini katika kikosi cha Amunike wapo Thomas Ulimwengu, ambaye hivi karibuni ilidaiwa amesitisha mkataba wake na Al Hilal ya Sudan kwa ajili ya ofa nono, Shaaban Iddi Chilunda anayekipiga CD Tenerife ya Hispania, Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana, nahodha wa Simba, John Bocco, na kinda Yahya Zayed wa Azam FC. Wachezaji hawa wote wana uwezo wa kucheka na nyavu.

Hiki ni kikosi kazi ambacho mapokezi ya kishujaa yanawasubiri endapo watawafunga Lesotho na kusubiri kumaliza shughuli nyumbani mapema mwezi ujao dhidi ya Uganda Cranes.

 

 

 

 

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*