KIKOSI CHA SIMBA CAF HIKI HAPA

*Haruna Niyonzima, Jjuuko ndani, Gyan, Kaheza ‘out’

NA MWANDISHI WETU

GAZETI la BINGWA limenasa orodha ya majina ya wachezajji 25 wa kikosi cha Simba watakaocheza katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika msimu huu.

Klabu hiyo ya Simba imepata nafasi hiyo ya kushiriki michuano hiyo ya Klabu Bingwa Afrika inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), baada ya kubeba taji la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.

Wakati Simba wanasubiri CAF wapange ratiba ya michuano hiyo na kujua mpinzani wao, tayari wamekwishaandaa kikosi ambacho kitaiwakilisha nchi kwenye michuano hiyo ya kimataifa kwa klabu.

Chanzo cha ndani kimeliambia BINGWA kuwa ni nyota watano pekee ambao ndio watakosekana katika orodha hiyo ya wachezaji 25 watakaokipiga michuano hiyo ya CAF.

“Wachezaji ambao hawatakuwamo kwenye kikosi hicho ni Gyan (Nicholas), Marcel (Kaheza) Nduda (Said Mohemed) Ally Salim na Mo Rashid (Mohamed Rashid),” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilisema si kwamba wamewaacha wachezaji hao kutokana na kutokuwa na uwezo la hasha, bali wamewaacha kwa kuwa wachezaji wanaotakiwa ni watano pekee.

Pia chanzo hicho kilisema kati ya wachezaji 25 ambao watakuwamo kwenye timu hiyo ni pamoja na kiungo wa Rwanda, Haruna Niyonzima, Adam Salamba na beki wa Uganda, Jjuuko Murshid.

“Niyonzima na Jjuuko wamejumuishwa kwenye kikosi hicho pamoja na wachezaji wengine,” kilisema chanzo hicho.

Wachezaji hao ni mlinda mlango, Aishi Manula, Deogratius Munishi ‘Dida’ na mabeki Shomari Kapombe, Asante Kwasi, Mohammed Hussein, Paschal Wawa, Erasto Nyoni, Yusufu Mlipili, Paul Bukaba na Salim Mbonde.

Viungo ni pamoja na James Kotei, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Shiza Kichuya, Cletus Chama, Hassan Dilunga, Mohammed Ibrahim, Abdul Hamis, Rashid Juma, Said Ndemla na washambuliaji ni Emmanuel Okwi, John Bocco na Middie Kagere.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*