googleAds

HANSPOPE AREJESHWA USIKU WA MANANE

NA SAADA SALIM,

MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, amerejea kundini ikiwa ni siku moja baada ya kutangaza kujiengua.

Hans Poppe aliamua kujiuzulu nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili kwa madai ya viongozi wa Simba kutomshirikisha katika mkataba wa miaka mitano wa udhamini wa klabu hiyo kutoka kwa kampuni ya SportPesa.

Lakini jana Pope alithibitisha kurejea Simba, akisema uamuzi wake huo umetokana na mkutano uliofanyika baina yake na wajumbe wa Kamati ya Utendaji, uliomalizika saa 9 usiku wa kuamkia jana.

Alisema kikao hicho kimemaliza suala lao na hivyo kuamua kurejea katika klabu hiyo kuendelea na majukumu yake.

“Kweli tumekutana, kuzungumza na kuweka sawa hili jambo, mwisho tumekubaliana na tumemaliza vizuri, huu ni wakati wa kusonga mbele,” alisema Hans Pope.

Wakati huo huo, Makamu wa Rais Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, amewatuliza mashabiki wao kwani wamepanga kufanya mazungumzo na mfadhili wao, Mohammed Dewji (MO) ili kumaliza utata uliopo kwa sasa.

Simba imejikuta katika zengwe na mfadhili wao huyo baada ya kuingia mkataba wa udhamini wa miaka mitano mwenye thamani ya Sh bilioni 4.96 na kampuni ya SportPesa bila kumshirikisha.

Akizungumza na BINGWA, Kaburu alisema: “Kuna mambo mengi ambayo hatuwezi kuyasema mpaka pale tutakapozungumza na Mo, kwani tukiyasema sasa, yanaweza kuathiri mazungumzo yetu, hivyo itakuwa busara kama tukiacha kwanza hadi pale tutakapokamilisha.

“Tunamtafuta Mo kuzungumza naye ili tuweze kuyamaliza masuala yote kwa kuwa alichokuwa akikihitaji ni kufahamu namna ya mkataba ulivyo, watu wanatakiwa kufahamu Mo ni mwekezaji na huu udhamini ni mambo mawili tofauti.”

Simba kwa sasa ipo katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini ikikabiliwa na changamoto ya aina yake kutoka kwa watani wao wa jadi, Yanga. Mbali ya ubingwa wa Bara, Simba pia inakabiliwa na mchezo wa fainali ya Kombe la FA utakaoiwezesha kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*