KIGOGO BAYERN ATAMBIA JEURI YA FEDHA

MUNICH, Ujerumani


 

MKURUGENZI Mkuu Mtendaji wa Bayern Munich, Karl-Heinz Rummenigge, ametambia jeuri ya fedha akizitisha timu pinzani akisema kwamba wanaweza kufanya usajili wa kutisha endapo watahisi jambo hilo linahitajika.

Msimu uliopita Bayern walitwaa ubingwa wa Bundesliga kwa mara ya sita mfululizo na walifanya hivyo kwa staili ya aina yake baada ya kumalizia ligi wakiwa mbele kwa pointi 21 dhidi ya timu iliyoshika nafasi ya pili, Schalke.

Tangu kipindi hicho vinara hao waliweza kumsajili nyota wa Schalke, Leon Goretzka, huku mastaa wake wengine,  Serge Gnabry na Renato Sanches, wakirejea kutoka walipokuwa wakikipiga kwa mkopo.

Huku Arturo Vidal, Douglas Costa, Sebastian Rudy na Juan Bernat, wakiwa wameshaondoka, lakini  Bayern bado inaonekana kuwa vizuri kifedha jambo ambalo linamfanya Rummenigge  kuwapasha wapinzani wake ili walitambue hilo.

“Tuliwauza Douglas Costa, Sebastian Rudy na Juan Bernat kwa fedha nzuri ambayo iliingia katika vitabu vyetu vya kumbukumbu,” kigogo huyo alikiambia kituo cha runinga cha FCB TV.

 

“Tuna vyanzo vingi vya mapato ambavyo tunaweza kuvitumia kufanya usajili. Endapo tutaona kuna ulazima itatufanya tujitose kimya kimya,” aliongeza kigogo huyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*