googleAds

KIFO CHA PAPA WEMBA, MKE AFUNGUKA…

NA NOAH YONGOLO,

NI Jumanne nyingine tena  mpendwa msomaji wangu wa kona ya Bolingo, bado tumejikita katika jiji la Kinshasa, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DR.

Leo nakukutanisha na mke wa aliyekuwa nguli wa rumba nchini humo, marehemu Papa Wemba ‘Mzee Fula Ngenge’.

Baada ya miezi kadhaa kupita tangu mumewe afariki, Marie Rose Lozolo, au kwa jina jingine mama Amazone, mke wa marehemu Papa Wemba anakutana na  waandishi wa habari na kufunguka mengi kuhusiana na mpendwa wake huyo.

Anaanza kwa kusema kuwa katika maisha yake ya miaka 45 ya ndoa na mumewe walipitia mambo mengi.

“Bado naona ugumu kuishi bila mume wangu kipenzi ambaye alikuwa ni mwanamuziki kamili, mpole sana.

“Awapo nyumbani ni nadra sana kumsikia akiongea hovyo, lakini awapo jukwaani ni mtu mwingine tofauti kabisa, kwani huko ndiko ilikuwa dunia yake,” anasema mwanamama huyo.

Anaendelea kusimulia kuwa, sehemu nyingine ambayo alikuwa akionyesha uchangamfu wa hali ya juu ni pale anapokuwa na jamaa zake.

“Nikiwepo mimi huwezi kumsikia akisema lolote, muda mwingi anakuwa kimya,’’ anasema.

Mama Amazone alifahamiana na Papa Wemba akiwa na umri wa miaka 15 tu, wakati marehemu mumewe alikuwa na miaka 20.

Anasema katika kipindi chote alichoishi na mumewe hakuwahi kujua kama mumewe alikuwa na hadhi kubwa hadi pale alipofariki.

“Wakati akiwa hai alikuwa akipenda kunitania mara kwa mara, akisema siku atakayofariki ndiyo nitajua hadhi yake, pia aliniambia angependa kifo chake kimkute akiwa kazini (jukwaani ), kwa kweli utabiri wake ulitimia,” anasimulia.

Anasema hakuwahi kuambiwa na Papa kama ana mke mwingine au watoto zaidi ya binti mmoja ambaye alimlea yeye aitwaye Kukuna.

Mama Amazone anasema ataendelea kupigania haki miliki ya marehemu mumewe, kwani ameacha kazi nyingi na kubwa.

“Mume wangu alikuwa na nyimbo nyingi sana, kuna nyingine alishawahi kunitungia akinitamkia maneno haya; “Nasali nini mpo nakoma mopaya, na motema nayo yebisa nga, yebaka bolingo emata nzete, boni lelo tokomi separer, ngai naleli ngo maboko ezangi Amazone, Wemba alingaka, ngai naleli maboko ezangi Amazone, Jules alingaka. (Tafsiri yake: Hebu niambie inakuwaje, najikuta kama mgeni moyoni mwako, fahamu kwamba penzi lina nguvu ya kuupanda mti hadi juu, vipi leo twafikia hadi kuachana! Nalia mie nalia kweli nammiss Amazone nimpendaye, mie Wemba nalia mie Jules, naimiss mikono niipendayo ya Amazone).

Anasema kabla ya kifo cha  mumewe, walikuwa jijini Paris nchini Ufaransa ambako alipatwa na homa akalazwa hospitali kwa muda wa siku 10.

Iligundulika kuwa alikuwa na malaria, baada ya kupata matibabu aliruhusiwa, lakini madaktari walimshauri apumzike kwa muda wa wiki nne.

Baada ya wiki nne kumalizika wakiwa Paris, waliamua kuongeza wiki mbili zaidi za mapumziko na baadaye kuingia studio kurekebisha kazi ya albamu yake mpya ambayo tayari imeshatoka, kisha kurejea jijini Kinshasa, Kongo DR.

Anaendelea kusimulia kuwa, waliwasili Kinshasa akiwa na afya njema kabisa na alikuwa akihudhuria mazoezini na vijana wake kama kawaida.

“Siku moja kabla ya safari ya Abidjan, tulikuwa na wageni nyumbani kwetu, baada ya wageni wetu kuondoka majira ya saa nne usiku nilimwona mume wangu anapanga nguo zake kwenye begi, nikamuuliza kulikoni?

Akaniambia anajitayarisha kwenda mazoezini usiku huo, kwani asingeweza kurudi nyumbani kwakuwa asubuhi alitarajia kusafiri  na vijana wake nchini Ivory Coast ambako angefanya shoo,” anasimulia mjane huyo.

Mama Amazone anasema hakufurahishwa na utaratibu huo, kwakuwa alihofia hatua ya mumewe kulala mazoezini kungeweza kumsababishia matatizo ya kiafya, hivyo alimshauri kuachana na mpango huo, lakini alikataa.

“Mazingira waliyokuwa wanafanyia mazoezi hayakuwa rafiki, yalikuwa na mbu wengi, ndiyo maana sikuafiki uamuzi wake na nikamshauri  alale nyumbani, lakini aligoma.

“Nakumbuka siku mume wangu anasafiri ilikuwa  Jumanne, ilipofika Ijumaa nikaenda kwenye ibada ya maombi, nikakaa huko mpaka Jumapili alfajiri ndio nikarudi nyumbani.

Ilipofika saa mbili asubuhi walikuja watu kuniamsha, huku wengine wakilia, nikajiuliza kuna nini? Wakaniambia mume wangu amefariki,” anasimulia kwa uchungu mama Amazone.

Baada ya hapo Serikali ya Kongo DRC ilimsafirisha hadi nchini Ivory Coast na kupokelewa na waziri wa utamaduni wa nchi hiyo, akiambatana na mawaziri wengine watatu pamoja na daktari maalumu wa kumuangalia iwapo litatokea tatizo lolote kwake.

MAKALA HII ITAENDELEA WIKI IJAYO. 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*