KICHWA CHINI, MIGUU JUU…Arsenal wangekuwa na kila kitu chini ya Abramovich


LONDON, England

KITABU cha maisha kinachomhusu mmiliki wa Chelsea kinaeleza kuwa Roman Abramovich, alihitaji kuinunua Arsenal wala si Chelsea mwaka 2003.

Ndani ya kitabu inaelezwa kuwa kumiliki timu ndani ya Ligi Kuu ya England ilikuwa kipaumbele kwa Abramovich ambaye alikuwa na uwekezaji mkubwa wa fedha katika Benki ya Swiss UBS, siri hiyo imetobolewa na waandishi wa kitabu hicho, Joshua Robinson na Jonathan Clegg.

Tajiri huyo alikuwa na ndoto kubwa za kuimiliki klabu ya Arsenal lakini taarifa zilidai kuwa, Washika Bunduki hao wa London hawauzwi kauli hiyo ilitoka kwa Mwenyekiti Msaidizi, David Dein.

Abramovich hakukata tamaa inadaiwa kuwa aliweka zaidi ya pauni milioni 250 kuinunua Arsenal, lakini bado dau hilo lilipigwa chini kwa mara nyingine.

Aliamua kuachana na timu hiyo, safari hii aliigeukia Tottenham kupitia kitabu hicho inaelezwa kuwa alienda na gari mpaka White Hart Lane lakini hakuridhishwa na mazingira ya pale.

Mazingira yalikuwa ya ovyo wala hakufikiria tena kuinunua klabu hiyo.

Kitabu kinadai kuwa alipokuwa njiani na gari kuelekea Tottenham, aliangalia nje kisha alisikika akisema kuwa: “Hapa ni pabaya kuliko Omsk.” Omsk ni sehemu ambayo zinatupwa takataka nchini Serbia.

Kwa hiyo alihamishia mawazo yake katika timu ya Chelsea na kufanikiwa kuinunua klabu hiyo kwa dau la pauni milioni 140 mwaka 2003.

Kuanzia hapo iligeuka kuwa historia, mataji manne ya Ligi Kuu ya England, makombe matano ya FA, matatu ya Carabao, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi ya Europa.

Sasa fikiria kama tajiri huyo angeinunua Arsenal ingekuwaje?

WENGER ANGEFUKUZWA 2004/05

Inafahamika kuwa, Abramovich huwa hajifikirii mara mbili anapotaka kufanya maamuzi ya kubadilisha kitu.

Unaambiwa waulize hata wanawake aliowahi kuishi nao. Ni sawa na makocha ambao wamewahi kufundisha Chelsea.

Ndani ya miaka 16 Stamford Bridge, timu hiyo imenolewa na makocha 15, wakati anaichukua klabu hiyo alimfukuza Claudio Ranieri ambaye aliiwezesha Chelsea kumaliza nafasi ya pili (nafasi ambayo mara ya mwisho walimaliza miaka 49 iliyopita).

Alimfukuza Carlo Ancelotti ambaye aliwapa taji la Ligi Kuu ya England na timu iliishia nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya huku wakiweka rekodi ya kufunga mabao 103 msimu ule.

Je, Arsene Wenger angevumiliwa licha ya kutwaa taji la Ligi Kuu ya England bila kufungwa msimu ambao Abramovich anainunua Chelsea?

Lakini msimu uliofuata Arsenal walitolewa hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya huku wakipitwa pointi 12 na Chelsea ambao walitwaa taji la Ligi Kuu msimu wa 2004/05.

Ndio, Wenger alishinda Kombe la FA msimu huo lakini isingemfanya asifukuzwe na Abramovich ambaye hufanya maamuzi magumu kila wakati.

MOURINHO ASINGEKUWA CHELSEA

Zamani, Chelsea ilikuwa inamilikiwa na Ken Bates ambaye aliinunua klabu hiyo mwaka 1982 kwa pauni 1 tu huku akiwa anamiliki na hisa nyingine za timu hiyo yenye maskani yake London, akisaidiwa na Matthew Harding estate, BskyB and several offshore trusts.

Mourinho alikuwa mmoja wa makocha waliotengeneza jina wakati huo akitoka kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Europa akiwa na FC Porto.

Hata hivyo, wamiliki wa Chelsea wakati huo wasingeweza kumwajiri Mourinho ambaye mshahara wake ulikuwa pauni milioni 4.2 kwa mwaka huku akiweka rekodi nchini England.

Ikiwa wakati huo Chelsea ilikuwa kwenye janga kubwa la vifaa hafifu vya mazoezi ndani ya uwanja wao wa mazoezi wa Harlington Complex.

Pesa haikuwa tatizo kubwa kwao kwani waliweza kuwaajiri akina Ruud Gullit, Gianfranco Zola na Gianluca Vialli, kwa levo yao lakini wasingeweza kuwa kivutio kwa makocha wakubwa wenye nguvu.

LAKINI ANGEENDA ARSENAL…

Baada ya yote, Arsenal walikuwa kwenye wakati mzuri kama kumiliki uwanja unaoingiza mashabiki 60,000, kwa kiasi kikubwa walikuwa na mashabiki huku wakiwa na uwezo wa kushinda mataji.

Ukichanganya na uwepo wa Abramovich kumwajiri Mourinho, lingekuwa suala la kawaida sana kwao bila kujali dau la mshahara ambao angeuhitaji wakati ule.

Arsenal na Mourinho wangeshirikiana kuongeza nguvu katika soko la usajili ikiwa mwaka 2004 Washika Bunduki walitumia pauni milioni 1.5 kumsajili Emmanuel Eboue katika dirisha kubwa la usajili.

Wakati huo, Mourinho alitumia pauni milioni 90 katika dirisha hilo la usajili kwa kuwasajili akina Arjen Robben, Petr Cech, Ricardo Carvalho na Didier Drogba.

MATAJI LUKUKI

Kwa miaka 16 ndani ya Chelsea, Abramovich ameshuhudia klabu yake ikitwaa mataji zaidi ya 10 ikiwa ni mataji mengi zaidi ya Arsenal.

Mataji manne ya Ligi Kuu ya England, makombe matano ya FA, matatu ya Carabao, Ligi ya Mabingwa na Ligi ya Europa.

Kwa maana hiyo, hayo mataji yote yangekuwa kwenye kabati la Arsenal kama Abramovich angekubaliwa kuinunua klabu hiyo wakati ule.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*