googleAds

KICHUYA MWINGINE APATIKANE KOMBE LA MAPINDUZI

NA WINFRIDA MTOI

KOMBE la Mapinduzi ni moja ya michuano yenye mvuto, kutokana na kushirikisha timu mbalimbali na inafanyika wakati ambao  Ligi Kuu ya Tanzania Bara imepamba moto.

Hali hiyo inazifanya timu za Bara  kuingia kwenye michuano hiyo zikiwa na  nguvu kubwa ya kutaka kuchukua kombe hilo ili kuwa na chachu ya kufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu Bara, pia timu za Zanzibar nazo zinakuwa na moto wa ligi yao.

Mara nyingi waandaaji wa michuano hiyo, huangalia zile timu zinazofanya vizuri na zenye upinzani  mkali ambapo mwaka huu timu za Bara zinazoshirki kombe hilo ni  Azam, Simba na Yanga.

Upinzani wa timu hizi zinapofika kwenye Kombe la Mapinduzi unakuwa wa hali ya juu zaidi ya ule wa kwenye ligi, hii ni kwa sababu kila mmoja anataka kuzima ngebe za mwenzake  hasa wale wanaofukuzia ubingwa wa Bara.

Tofauti na upinzani uliopo, michuano hii hufanyika kipindi ambacho timu hizi zote zimetoka kufanya usajili wa dirisha dogo hivyo kutumia mashindano hayo kuwapima wachezaji wao wapya waliowasajili kwa wakati huo.

Naamini unakuwa ni wakati mzuri kwa wachezaji waliokuwa hawapati nafasi na wale wapya kuonekana kutokana na makocha wa timu hizi kuwapa kipaumbele zaidi.

Michuano ya Mapinduzi iliyopita, tuliona wachezaji kama Shiza Kichuya, Mohamed Ibrahim, Mzamiru Yassin, Andrew Vincent na wengine, walichokifanya wakati wakiitumikia Mtibwa Sugar, lakini Antony Matheo (KMKM).

Wachezaji hawa waling’ara kwenye michuano ya Mapinduzi na hadi waliporudi Ligi Kuu viwango vyao viliendelea kuwa juu kitendo kilichowafanya viongozi wa timu  za Simba na Yanga kuwatolea macho na mwisho wake kuwasajili.

Hii inaonyesha jinsi gani mashindano haya yalivyo na uwezo mkubwa wakuvifanya viwango vya wachezaji kuonekana zaidi hasa kutokana na changamoto iliyopo kwenye mashindano ya kuzikutanisha timu zinazoshiriki ligi za nchi tofauti na kucheza mechi kila baada ya siku moja.

Wapo wachezaji wengi ambao hawakuonekana kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi, huu ni wakati wao sasa kupewa nafasi ya kuonekana kwa kuwa naamini wapo akina Kichuya wengi watakaoweza kuondoa ile dhana ya kuamini wachezaji wa kigeni pekee.

Kwa mfano wachezaji kama Pastory Athanas alisajiliwa na Simba na Emmanuel Martin wa Yanga huu ni wakati wao wa kuwaonyesha mashabiki wa timu hizi kwamba hawajapotea njia kuwasajili kwa kupewa nafasi yakucheza kila mechi.

Kitendo hicho kitawafanya kuwa pamoja na kuwazoea wenzao ambao wamekaa nao kwa muda mfupi tangu wamesajiliwa. Yupo pia Shaabani Iddi wa Azam FC ambaye ameifungia bao timu yake katika mechi ya kwanza na Joseph Mahundi aliyesajiliwa na Azam hivi karibuni akitokea Mbeya City.

Hivi sasa mashabiki wa timu zote macho yao yako Zanzibar kuangalia  ni vitu gani vitafanywa na wachezaji  wapya na wanaweza kuwapiku wale waliokuwepo au ndiyo mambo yatakuwa yale yale kama ilivyo kwa baadhi ya wageni waliosajiliwa kwa mbwembwe nyingi lakini hakuna kikubwa walichokifanya.

Mashabiki wengi wa soka ni watu wanaopenda raha siku zote, wanapenda kuona usajili uliofanywa na timu zao unaleta mafanikio, kinyume na hapo lazima wapige kelele.

Katika kikosi cha Simba, usajili wa awali wa msimu huu kwa wazawa hakuna tatizo kwa sababu kina Kichuya wanaonekana vitu wanavyovifanya.

Kwa upande wa Yanga yupo, Andrew Vincent ‘Dante’ pekee ndiye aliyeweza kuonyesha uwezo huku mchezaji aliyesajiliwa kwa fedha nyingi, Obrey Chirwa, akiwa bado hajaonyesha kile kilichotarajiwa na wengi.

Kipimo cha wachezaji  waliosajiliwa mwanzoni mwa msimu huu, kimeonekana kwenye mechi 15, kibarua kilichobaki ni kwa wale walioingia  kwenye timu hizi Desemba mwaka jana,  kwani kila mtu ana hamu ya kujua walichonacho.

Kama ilivyokuwa kwa Kichuya na wachezaji wengine wazawa kung’aa, sasa ni zamu ya Pastory Athanas aliyesajiliwa na Simba na Emmanuel Martin wa Yanga kuonyesha uwezo kwenye michuano hii waweze kuaminika zaidi kwenye vikosi na mashabiki wao.

Viwango walivyoonyesha kwenye timu zao walizotoka ndivyo vilivyowafanya wapate nafasi ya kusajiliwa na timu hizi kubwa ambapo Athanas alitokea Stand United na Martin JKU ya Zanzibar.

Katika mechi tatu za ligi za duru ya pili kabla ya kuelekea Zanzibar, wachezaji hawa walipewa nafasi ya kucheza kwenye vikosi vyao vipya na kuonyesha viwango vizuri.

Hiyo haitoshi, matumaini ya mashabiki wengi ni kuendelea kuona wachezaji hawa wanafanya vizuri michuano hiyo ili kujiaminisha kuwa wamesajili vifaa vinavyostahili kuchezea timu zao.

Si hilo tu, pia michuano ya Mapinduzi itaweza kuwaongezea uzoefu wachezaji hawa wa kuendana na mfumo wa makocha wa klabu hizo zenye ushindani wa namba kama alivyothibitisha Athanas.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*