KATAA HALI HII, HAYA SI MAHUSIANO UNAYOSTAHILI

NA RAMADHANI MASENGA


KUNA wengi wakipita mitaani wanachekwa kisa mapenzi. Wengine imepelekea kufukuzwa kazini kwa ufujaji wa fedha, kisa mapenzi.

Mapenzi yamewafanya baadhi ya watu kuishi katika aina ya maisha ambayo hawajawahi hata kuyaota. Katika hili ndiyo maana msemo dhaifu wa mapenzi mabaya huwa unazuka.

Mapenzi si mabaya ila kuwa watu wenye akili mbaya wanatumia mapenzi katika malengo mabaya na kufanya uamini tofauti juu ya maana ya mapenzi. Unaishi vipi na mpenzi wako?

Hiyo furaha tunayokuona nayo usoni ipo mpaka moyoni? Hizo safari za kila siku Zanzibar kwa ajili ya kubadilisha hali ya hewa uko radhi nazo? Wengi wanacheka usoni huku wakilia moyoni.

Unamuona anatoa fedha akisema honey usijali huku nafsi yake ikisikitika. Inavuja damu kwa sababu anajikamua kutoa kwa ajili ya kumridhisha mwenzake hali nafsi yake haijaridhi.

Mapenzi yanafaa kukupa amani na raha katika maisha yako. Ukiona mwenzako anatumia upendo wako kama silaha ya kukutesa huyo hakufai.

Kuna dada mmoja alikuwa akinisimulia mahusiano yake yaliyopita. Katika maongezi yangu na yake yaliyodumu takribani dakika kumi na tano, niligundua ugonjwa ambao wengi wanaugua, alisema hivi:

“Nilikuwa na mvulana ambaye nilimpenda sana. Kutokana na mvuto aliokuwa nao nilijitahidi kumfanyia mambo mengi makubwa ili nisitoe nafasi kwa wengine kumpata.

Nilijitahidi kumtimizia kila kitu alichokuwa anakitaka, mambo ambayo nilikuwa namfanyia hata ndugu zangu sijawahi kuwafanyia.”

“Nilimpa fedha nyingi, kumnunulia mavazi ya gharama na kila siku nilikuwa nahakikisha nampa fedha ya matumizi madogo madogo.”

“Wakati mwingine nilikuwa radhi kumpa fedha nyingi na mimi kubaki na kidogo. Yote  niliyafanya kwa mapenzi yangu juu yake. Ila pamoja na yote hayo, mpenzi wangu hakuonesha kujali.

Alifanya karibu kila nililokuwa nalichukia, alininyanyasa kadiri alivyopenda. Nikaishia kulia na kuvumilia kwa sababu nilimpenda sana.”

“Nilijitahidi kuvumilia kwa sababu niliogopa kumkwaza na kupekelekea tukaachana. Nilijiuliza ningempata wapi kama yeye?

Mwenye muonekano bora kama yeye ambaye kila nikipita naye wanaume walikuwa hawaishi kumtazama kwa matamanio! Kila nikifikiria hilo nikajikuta nikiwa tayari kuvumilia madhila yake na maisha kuendelea,” Tuishie hapo!

Huo ni mfano mmoja, ila wengi wanaugua ugonjwa wa namna hiyo. Akili zao zinashindwa kuamini kuwa ni bora kuishi bila mnke/ mume kuliko maumivu ya kuishi na mtu asiye na hisia na wewe.

Kutokana na hilo, ndiyo maana wajinga wachache baada ya kuona udhaifu huo  wanawageuza miradi ama vijakazi wao. Kila kitu anataka yeye, kila nguo anataka avae. Si anajua mwenzake utajipinda tu na kutimiza! Sasa afanye nini?

Huu ni zaidi ya utumwa unaoujua. Amini wewe ni bora. Kama yeye anashindwa kuuona ubora wako, wako wengine watakaouona na kuuheshimu.

Kuishi na mtu mwenye muonekano unaovutia wengi ila anakufanya ulie kila siku haipishani sana na mwili wa jambazi kubebwa katika jeneza la dhahabu. Haina maana!

Sasa kwanini ukubali sifa za nje wakati ndani unaumia. Acha ujinga, amka na amua kuwa mtu halisi kuanzia sasa. Heshimu mwili wako, malengo yako na furaha yako katika maisha.

Huyo unaemthamini na yeye hajali atakusababishia maumivu na kushindwa kufanya mambo yako mengine. Wakati mwingine inabidi ukubali ni bora kuishi Sudani uraiani kuliko Marekani ndani ya gereza.

Yeye kila siku anataka pesa, nawe unatoa tu, akitaka hiki unampa akitaka kile unampa, kisa? Ukisema huna atakuacha. Sasa hayo mapenzi kweli?

Jiamini wewe, uliyenye si mtu mwema kwako. Si ajabu unachompa anaenda kula na ampendaye. Wewe upo tu. Kazi yako ni kutafuta na kutoa, wanatumia wale kule. Halafu na bado kwenye simu ‘umemsevu’ sweetie!

Ukiamua kujiamini utampata akupendaye na aliye bora kuliko huyo anayekutumia. Wewe ni bora na unayefaa kuthaminiwa, achana na mawazo ya kuamini huyo ni bora zaidi.

Amini bila yeye utasonga na kufika pale unapotaka ufike. Katika maisha silaha kubwa ni kujiamini. Utathaminiwa kwa sababu ya kujiamini na utadharaulika kwa sababu ya kutojiamini. Ahsanteni sana!

ramadhanimasenga@yahoo.com


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*