googleAds

KASEKE YULEE WA MBEYA CITY ANUKIA

NA MICHAEL MAURUS

KIUNGO wa Yanga, Deus Kaseke, amezidi kuwa ‘mtamu’ kadri siku zinavyokwenda, akifanya mambo makubwa katika mazoezi yanayoendelea kwenye Uwanja wa Chuo cha Biblia, mjini hapa.

 Mwanzoni wakati anatua Yanga, akitokea Mbeya City, Kaseke alikuwa ni habari nyingine kutokana na uwezo wake wa kukaba, kupoka mipira na kuipa presha ngome ya wapinzani, akibebwa zaidi na kasi na nguvu zake.

Uwezo wake huo pamoja na wachezaji wenzake, ndio uliochangia Mbeya City kuwa tishio enzi hizo, ikizitoa jasho timu pinzani, wakiwamo wakongwe wa soka nchini, Simba na Yanga, hasa inapocheza kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Sokoine, Mbeya.

Kaseke aliendeleza makali yake hata alipotua Yanga mwaka 2015, akisajiliwa ili kuziba pengo la winga hatari wa Wanajangwani hao, Mrisho Ngassa, aliyetimkia Free State Stars ya Afrika Kusini, akiiwezesha timu yake hiyo mpya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Lakini kadri siku zilivyozidi kwenda kiwango cha Kaseke kilizidi kushuka, akishindwa kuendeleza cheche zake, hata alipotua Singida United na hadi aliporejea Yanga msimu uliopita.

Lakini kutokana na ujio wa wachezaji wapya Jangwani, safari hii Kaseke ameonekana kuchachamaa mazoezini ili kurejesha makali yake, kama anavyofanya mwenzake Ngassa ambaye tayari ameshaanza kuwa tishio.

Si BINGWA pekee lililobaini cheche za Kaseke mazoezini mjini hapa, bali hata Mwenyekiti wa Yanga, Dkt. Mshindo Msolla, ameliona hilo alipotembelea kambi ya timu hiyo juzi.

Akizungumza na BINGWA baada ya mazoezi yaliyoambatana na mechi ya kirafiki dhidi ya Moro Kids wiki iliyopita, Dkt. Msolla alisema: “Ninamuona Kaseke yule wa Mbeya City akirejea, anapambanahasa. Niliwahi kuuliza ‘yule Kaseke wa Mbeya City yuko wapi?’ Nadhani alinielewa na ameanza kurejesha kiwango chake.”   

Mbali ya Kaseke, wachezaji wengine waliokuwapo kikosini Yanga msimu uliopita ambao wanaonekana kujifua vilivyo kusaka namba baada ya ujio wa nyota wapya, ni Paul Godfrey ‘Boxer’, Ngassa, Mohammed Issa ‘Mo Banka’, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Said Juma Makapu na kadha wa kadha.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*