googleAds

Kaseja awekwa kiporo Simba

MWAMVITA MTANDA NA PENDO HAMISI (TUDARCo)

KUTOKANA na kazi kubwa aliyoifanya katika mchezo wa kuwania kutinga makundi ya kusaka tiketi ya fainali za Kombe la Dunia 2022, kipa wa Taifa Stars, Juma Kaseja, amewekwa kiporo na Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, aliyekiri kutamani kufanya kazi na nyanda huyo.

Kaseja aliibania Burundi katika mchezo dhidi ya Stars wikiendi iliyopita, akidaka penalti ya kwanza iliyoonekana kuwanyong’onyesha wapinzani wao hao na kukosa nyingine mbili.

Akizungumza na BINGWA jana, Aussems alisema anapenda namna kipa huyo anavyofanya kazi yake kwa ufanisi, hivyo si vibaya kama siku moja atarudi Simba aliyowahi kuidakia kwa mafanikio makubwa miaka ya nyuma.

Alisema kuwa kwa jinsi alivyofuatilia mechi za kipa huyo, amemwona kama mchezaji mwenye nguvu japo anaelezwa kuwa na umri mkubwa.

“Mchezaji bora hapimwi kwa umri bali namna ambavyo anafanya kazi yake, tangu nimeanza kumfuatilia Kaseja, kiukweli anafanya vizuri tena kwa kujiamini.

“Kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu mimi sioni kama ni mchezaji tu, bali ni zaidi ya mwalimu,” alisema Aussems.

Aussems alisema timu kumbwa kama Simba, ikifanikiwa kumchukua kipa huyo, itamfanya azidi kujiamini katika kazi yake.

Alisema kuwa jambo analoamini katika soka, kipa mwenye umri mkubwa ndio anaweza kudaka vizuri kutokana na uzoefu wake.

“Kwa sasa Kaseja ni kama nembo ya soka la Tanzania kwa makipa, waendelee kumtumia katika michuano ya kimataifa, kwa kuwa tayari alishajijengea sifa hivyo timu nyingi lazima zimuhofie, hali ambayo itaendelea kuipa ushindi Taifa Stars,” alisema Aussems.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*