googleAds

Karia kuwakomalia makocha, maproo

NA ASHA KIGUNDULA

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, amesisitiza kuwa makocha na wachezaji wa kigeni waliokwenda nchini kwao, wakirejea watawekwa karantini kwa wiki mbili.

Baadhi ya makocha na wachezaji hao wameondoka nchini, baada ya Serikali kutoa agizo la kusimamisha shughuli za mikusanyiko ya watu ikiwamo Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na tahadhari ya virusi vya Corona.

Akizungumza na BINGWA jana, Karia alisema hatabadili msimamo wake kwa wachezaji waliondoka nchini, wakirejea watakaa karantini wa wiki mbili chini ya uangalizi maalumu wa wataalam wa afya.

Alisema ameshangaa kusikia kuna baadhi yao wamekwenda katika nchi zao, wakati hakuna mchezaji wala kocha aliyepewa ruhusu ya kutoka nje ya Tanzania.

Rais huyo alisema kama walitoka nje ya nchi kwa kuvuka mipaka kwa kipindi hiki ligi zimesimama, watakutana na kizuizi.

Karia alisema Rais Jamhuri ya Muungano Tanzania, John Magufuli, jana alizungumza na Watanzania na wageni hakuna mtu kutoka hata ikiwezekana kwenda mikoani kama hauna shughuli maalum ya kufanya huko.

“Hakuna ambaye amepewa ruhusa ya kuondoka nje ya nchi, kwani sio likizo bali ni sitisho kwa muda kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya virusi ya Corona.

“Kocha ama mchezaji ambaye ametoka nje ya nchi hataruhusiwa kujiunga na wenzake mpaka akae sehemu maalum ambayo atajilipia kila kitu,” alisema Karia.

Wachezaji walioondoka baada ya Ligi Kuu Bara kusimamishwa ni Haruna Niyonzima na David Molinga na kocha Luc Eymael wa Yanga.

Meddie Kagere, Clatous Chama, Sharaf Shiboub na Luis Miquissone wa Simba.

Wachezaji wa Azam ni Razak Abalora, Nicolas Wadada, Bruce Kangwa, Mohammed Yakubu, Danny Amola, Donald Ngoma na Never Tigere na makocha wao, Vivian Bahati na Aristica Cioaba.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*