googleAds

KAMATI YA UFUNDI YANGA YAMPA MBINU MPYA ZAHERA


NA ASHA KIGUNDULA

KAMATI ya Ufundi Yanga imemtuliza mzuka Kocha Mkuu wa timu hiyo Mwinyi Zahera kwa kumwambia achape kazi kwa raha zake kwani bado wana imani naye na ajielekeze kufanyia kazi udhaifu mdogo uliopo katika kikosi chao.


Kauli ya Kamati hiyo imekuja siku chache baada ya kuwepo taarifa za baadhi ya wanachama na viongozi kutaka Kocha huyo atupiwe virago kisa ni mwenendo mbaya wa timu hiyo.


Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Klabu hiyo, Salum Rupia,amesema, bado wana imani na Zahera licha ya kuyumba kwa timu hiyo katika baadhi ya mechi kwani anayafanyia kazi madhaifu yote ya kikosi chake.


Alisema, wana imani na Kocha huyo atawafanyia makubwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya Kimataifa ambapo Kamati yake imejipanga kumpa ushirikiano wa nguvu ili kutimiza ndoto za kuona timu hiyo inawapoka maahasimu wao Simba ubingwa na kufanya vyema Kombe la Shirikisho Afrika.


Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati hiyo Charles Boniface Mkwasa, amesema ni mapema mno kwa Yanga kukata tamaa na Zahera wakati Ligi bado mbichi hivyo kushauri kumpa muda awasukie kikosi chaao.
Alisema,Zahera ni kocha mzuri mwenye uwezo wa kuwafanya makubwa endapo atapewa muda wa kuendelea kuinoa timu hiyo.


Alisema yeye kama kocha na mchezaji wa zamani wa Yanga na timu ya taifa, anaona Zahera bado anahitajika Yanga, kinachotakiwa kila Mwanayanga kuamini kuwa wana kocha mzuri na ana uwezo wa kufanya vizuri katika timu yao.


“Ni mapema sana kukata tamaa, kwa kuwa hata nusu ya mechi za Ligi Kuu hazijachezwa hivyo wakati wa kuona timu imefanya vibaya si sasa,”.
Mkwasa alisema, kila kocha anatambua anapofanya vibaya katika mchezo aliocheza hufanyia kazi mapungufu na hivyo Zahera anatambua jukumu lililo mbele yake ni kuwapa raha mashabiki wa timu hiyo.


Akizungumzia fununu za Wanayanga kutaka apewe kijiti endapo Zahera ataondolewa Mkwasa alisema,yeye yupo Kamati ya Ufundi kama mshauri, na kitu kama hicho kwake hakiwezekani.


Katika hatua nyingine Kocha Zahera ameliambia DIMBA Jumatano,kuwa licha ya kutopata matokeo ya kuridhisha katika michezo yao miwili ya ligi lakini anafanyia kazi udhaifu wa safu ya ushambuliaji na ukuta ili uwe wa zege ili kuhakikisha Yanga inakuwa na makali yake kwenye ligi na hata michezo ya kimataifa.


Alisema, bado ana kazi kubwa kwa upande wa mastaika yake kwa kuhakikisha anawapika ili waweze kupata mabao mengi zaidi kwa kila mchezo ulio mbele yao.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*