googleAds

Kakolanya: Nitampoteza vibaya Manula

NA ZAINAB IDDY  

SAA chache baada ya Simba kusambaza picha zinazomwonyesha Benno Kakolanya kusaini mkataba na Wekundu wa Msimbazi hao, kipa huyo ameahidi kumpoteza mpinzani wake, Aishi Manula.

Tetesi za Kakolanya kusaini mkataba Simba, zilianza kuvuma muda mrefu, lakini hatimaye jana Wekundu wa Msimbazi hao wamevunja ukimya na kuthibitisha kumpa mkataba wa miaka miwiki ‘nyanda’ huyo.

Akizungumza na BINGWA jana, Mtendaji wa Mkuu wa  Simba (CEO), Crescentius Magori, alisema kuwa huo ni mwendelezo wa kuwaonyesha Wanasimba wachezaji ambao ni mali yao kuelekea msimu ujao.

“Jana (juzi) nilisema katika mkutano wangu na vyombo vya habari kuwa tumeshakamilisha usajili wetu kwa zaidi ya asilimi 90, ikiwemo kuongeza mikataba ya wachezaji wetu muhimu ambao kocha amehitaji kuendelea nao.

“Usajili huu wa Kakolanya na wengine, unalenga zaidi mashindano ya kimataifa yaliyopo mbele yetu na ndio maana kila nafasi tunakuwa na wachezaji zaidi ya wawili.

“Kila siku tutakuja na mtu mwingine, Wanasimba wasiwe na shaka tunafanya kazi kwa umakini mkubwa kwa kufuata matakwa ya kocha wetu ambaye ndiye mwenye jukumu la kuipa matokeo chanya timu.”

BINGWA lilimtafuta Kakolanya ambaye alikiri kusaini mkataba Simba, akisisitiza kufanya hivyo ili kupata ushindani ambao hakuwa akiupata akiwa Yanga.

“Nitafanya kazi Simba kwa misimu miwili, najua kuna ushindani wa namba na inaweza kuwa vigumu kumuweka benchi Manula (Aishi), lakini naenda nikiwa najua nitatakiwa kupambana ili kuwa bora zaidi yake kwa kuwa nahitaji   nipate nafasi ya kucheza, hivyo lazima nitafute namna ya kuwa bora zaidi ya wenzangu (Manula na Deogratius Munish ‘Dida),” alisema Kakolanya. 

Aliongeza:  “Yanga nilikuwa namba moja, sikuwa napata ushindani, kitu ambacho kilinifanya nione nipo bora, kumbe nilijidanganya, lakini uwepo wa Manula Simba, utanifanya nipambane zaidi ili niwe bora zaidi na kumpora namba.”

Mwishoni mwa mwaka jana, Kakolanya aliomba kuvunja mkataba na Yanga, kutokana na kutoelewana na kocha wake, Mwinyi Zahera, aliyechukizwa na kitendo cha kipa huyo kususa kutokana na madai yake ya mshahara na fedha za usajili.

Tangu alipoanza kuwa na matatizo na Yanga, Kakolanya alikuwa akitajwa kujiunga na Simba, tetesi ambazo hatimaye zimethibitishwa ramsi jana na Wekundu wa Msimbazi hao.

Kutua kwake Simba,  kunamfanya kuwa mchezaji wa tano kusaini mkataba Msimbazi, wengine wakiwa ni Manula, John Bocco, Jonas Mkude na Erasto Nyoni.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*