googleAds

Kagere, Miraj waiua Mtibwa Sugar

NA WINFRIDA MTOI

KAMA kawa, kama dawa; kikosi cha Simba kimeendeleza wimbi la ushindi kwa wapinzani wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya jana kuichapa Mtibwa Sugar mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, huku Meddie Kagere na Miraj Athumani wakiibuka mashujaa wa Wekundu wa Msimbazi hao.

Huo ni ushindi wa pili mfululizo katika ligi hiyo uliowawezesha kufikisha pointi sita, ikiwa ni baada ya kuichapa JKT Tanzania mabao 3-1 kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wao, hii ni mara ya pili kwa Kagere na Miraj kuibeba Simba kwani hata katika mchezo uliopita dhidi ya JKT Tanzania, ndio waliotikisa nyavu, ‘MK 14’ akitikisa nyavu mara mbili. 

Ukiachana na Kagere na Miraj walioipa Simba ushindi, kiungo wa timu hiyo, Sharaf Shiboub, alikaribia kufunga bao maridadi kama lililowekwa kimiani na Clatous Chama katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita dhidi ya Nkana ya Zambia.

Shiboub akiwa ndani ya eneo la hatari, alipokea pasi ya chini chini kutoka wingi ya kushoto na kuupiga kwa kisigino kumfunga kipa wa Mtibwa Sugar, Shaaban Kado, lakini kabla haujavuka mstari, Kagere aliuwahi na kuusindikiza zaidi nyavuni.

Baada ya kosa kosa kadha wa kadha, Kagere ndiye aliyeanza kuipa Simba bao la kuongoza dakika ya 17 kutokana na kazi hiyo safi ya Shiboub, kabla ya Miraj kuongeza la pili dakika ya 68.

Miraji alifunga bao hilo akitokea benchi baada ya kuunganisha nyavuni pasi murua kutoka kwa Shiboub aliyeng’ara mno jana.

Kwa upande wao, bao la kufutia machozi la Mtibwa Sugar, lilifungwa dakika ya 20 na Riphat Hamis, akiunganisha kwa kichwa kona iliyochongwa na beki wa kushoto wa timu hiyo, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’.

Kwa ujumla mchezo huo ulikuwa mkali na wenye msisimkoa kwa muda wote wa dakika 90, huku kila timu ikionyesha kiu ya kusaka mabao tangu dakika ya kwanza.

Walikuwa ni Simba walioanza kulitia majaribuni lango la Mtibwa baada ya kiungo wao, Chama kupata nafasi ya kufunga dakika ya saba, lakini akashindwa kuitumia baada ya shuti lake kutua mikononi mwa Kado.

Dakika ya 15, Tshabalala alipiga krosi safi langoni mwa Mtibwa, lakini Kagere alishindwa kuiwahi na Kado kuondosha mpira eneo la hatari.

Kipa wa Simba, Aishi Manula, alifanya kazi ya ziada kuokoa shuti kali lililopigwa na Ally Yusuph dakika ya 34 na kuwa kona butu.

Abdulharim Humud wa Mtibwa, alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 45 na mwamuzi wa mchezo huo, Ally Simba kwa kumfanyia madhambi Shiboub.

Mzamiru Yassin, aliikosesha Simba bao dakika ya 52, baada ya kushindwa kuitumia pasi murua kutoka kwa Shiboub.

Dakika ya 90, Salum Kanoni wa Mtibwa Suga, alioneshwa kadi ya njano kwa kumfanyia madhambi, Miraj.

Baada ya mchezo huo, wachezaji wa Simba walisherehekea siku ya kuzaliwa ya kocha wao wa viungo, Mtunisia Adel Zrane na Manula, wakiwakimbiza uwanjani hapo na kuwamwagia mchanga.

Kikosi cha Simba: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Tairone Santos, Gerson Fraga, Clatous Chama/Francis Kahata (dk80), Mzamiru Yassin, Meddie Kagere, Sharaf Shiboub/Jonas Mkude (dk89) na Hassan Dilunga/Miraj Athumna (dk68).

Kikosi cha Mtibwa: Shaaban Kado, Salum Kanoni, Issa Rashid, Cassian Ponera, Dickson Daud, Abdulharim Mohammed, Ismail Mhesa/Abdul Haule (dk80), Ally Yussuph, Riphat Hamisi, Awadh Juma na Haruna Chanongo/Omary Hassan (dk67).


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*