KAGERE: HII NI RASHARASHA, MAMBO MAZURI YANAKUJA

TIMA SIKILO NA SALMA MPELI


MSHAMBULIAJI mpya wa timu ya Simba, Meddie Kagere, ametamba kuwa uwezo waliouonyesha jana katika mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana ni kama mvua za rasharasha, mchezo mzima utaonekana katika Ligi.

Simba juzi walitoa sare ya kufungana 1-1 dhidi ya Asante Kotoko, katika tamasha lao la Simba Day la kutambulisha wachezaji wa timu na viongozi wake.

Akizungumza na BINGWA jana, mshambuliaji huyo alisema matokeo yalikuwa ni ya kawaida, kwani mchezo ulikuwa ni wa kirafiki na si wa kutumia nguvu kubwa kama ambavyo inatakiwa kutumika katika michuano mingine.

Alisema kutoa sare katika mchezo wa kirafiki si kitu kikubwa sana, kwani ile ilikuwa ni katika kumfanya mwalimu kugundua mapungufu yaliyopo katika kikosi chake na kuyarekebisha ili kuyaepuka katika michezo mingine.

“Ile ilikuwa ni mechi ya kirafiki sawa na mazoezi, lakini tulikuwa vizuri na nina imani timu ikikaa pamoja kwa muda mrefu tutafanya vizuri zaidi,” alisema.

Katika hatua nyingine, Kagere alisema hamasa kubwa iliyoonyeshwa na mashabiki wa klabu hiyo juzi kwenye tamasha la Simba Day imemfanya kujiona ana deni kubwa mbele ya mashabiki hao kwenye Ligi.

Alisema wingi wa mashabiki hao waliojitokeza kuisapoti timu yao uwanjani hapo, umempa picha ya namna gani wanahitaji mafanikio makubwa katika Ligi, huku kubwa kwao kama wachezaji ni kuhakikisha sasa wanajituma zaidi ili kufanikisha timu hiyo kutetea taji lao la Ligi hiyo, lakini pia kufika mbali katika michuano ya kimataifa.

“Simba Day ni siku kubwa, lakini hamasa ya mashabiki waliokuja uwanjani kutoa sapoti kwa timu ni ishara tosha ya kutegemea mafanikio makubwa ya klabu yao katika Ligi na hata kwenye michuano ya kimataifa,” alisema Kagere.

Simba, ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Bara, wanatarajiwa kufungua pazia la Ligi Kuu kwa mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Mtibwa Sugar, ambao ni mabingwa wa kombe la FA, mchezo utakaopigwa Agosti 18, mwaka huu, katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Kikosi cha timu hiyo kilichorejea hivi karibuni kutoka kambini nchini Uturuki, kwa sasa kinaendelea na mazoezi yake kwa ajili ya mchezo huo na michuano ya Ligi Kuu itakayoanza Agosti 22, mwaka huu, dhidi ya Tanzania Prisons, katika Uwanja wa Taifa,  jijini Dar es Salaam.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*