googleAds

Kagere avunja ukimya

Tima Sikilo

MSHAMBULIAJI wa Simba, Meddie Kagere, amewapoza mashabiki wa timu hiyo wanaotilia shaka kasi yake ya kufunga mabao akiwataka kuwa na subira kwani mambo mazuri yanakuja.

Mashabiki na wapenzi wa Simba wamekuwa wakimzungumzia mchezaji huyo kutokana na kitendo cha kuzorota kwake katika kufunga mabao tofauti na alivyokuwa mwanzoni mwa msimu huu.

Kagere ana jumla ya mabao 11 katika michezo 16 waliyocheza msimu huu.

Akizungumza na BINGWA jana, Kagere alisema huwa hapendi kuongea zaidi ya kuonyesha cheche zake kwa vitendo uwanjani.

Hata hivyo, alifafanua kuwa bado hayupo mbali na rekodi yake ya msimu uliopita kwani ndani ya michezo 15, alikuwa na mabao tisa, wakati hadi sasa akiwa ameshuka dimbani mara 16, ana mabao 11.

“Sidhani kama kuna tofauti kubwa kati ya msimu huu na msimu uliopita, hivyo mashabiki wasiwe na hofu na mimi, niko sawa.

“Waangalie zaidi rekodi zilivyo wataelewa kuwa hakuna tofauti yoyote iliyopo,” alisema

Kagere anaongoza kwa mabao katika wafungaji wa Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na mabao yake hayo 11, akifuatiwa na Paul Nonga wa Lipuli mwenye mabao nane.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*