googleAds

Kabwili afanya miujiza, Manyika hoi

NA MICHAEL MAURUS

KIPA wa Yanga, Ramadhan Kabwili, ameendelea kufanya miujiza mazoezini, akionyesha vitu adimu vilivyowaacha hoi wengi, kuanzia makocha wake, akiwamo wa makipa, Peter Manyika, mashabiki hadi wachezaji wenzake.

Akiwa lango wakati wa mechi mazoezi, Kabwili aliyesajiliwa kama mchezaji wa kikosi cha vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Under 20), alikuwa akiokoa michomo ya hatari kutoka kwa washambuliaji kama Juma Balinya, Sadney Urikhoub, Patrick Sibomana, Lamile Moro, Said Juma Makapu na wengineo.

Kinda huyo mkazi wa Tabata Twiga, alianza kugomea akina Balinya wakati wa zoezi la kupiga mashuti kwa miguu yote miwili, lililowahusisha wachezaji wote.

Baada ya kugawa vikosi viwili kucheza uwanja mzima, Kabwili alifanya matukio mawili ambayo ndiyo yaliyowashangaza wengi.

Wakati vikosi hivyo vikiwa vinajipanga tayari kuanza mechi ya wenyewe kwa wenyewe, alipopigiwa mipira ya juu kimo cha mbuzi na Manyika, Kabwili alikuwa akilala na kuirudisha ilikotoka kwa visigino, akifanya hivyo kwa staili ya ‘tik taka’, ukiwa ni mtindo ulioasisiwa na kipa wa zamani wa Colombia, Rene Higuita.

Higuita alianza kufanya hivyo katika mchezo wa kirafiki kati ya Colombia na England, Septemba 6, mwaka 1995, ikiwa ni kutokana na shuti la Jamie Redknapp, tukio lililovuta hisia za wengi na kupewa jina la ‘scorpion kick’.

Kabwili amefanya hivyo ikiwa ni siku moja tangu alipoonyesha uwezo wake wa kufunga mabao, wakati wa mazoezi ya juzi asubuhi, akicheka na nyavu mara mbili, likiwamo bao maridadi la kichwa cha kuruka (diving head).


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*