KABUNDA AZIVURUGA SIMBA, AZAM

NA SAADA SALIM,

WINGA Hassan Kabunda anayekipiga kwenye klabu ya Mwadui FC, amewavuruga mabosi wa Simba na Azam ambao wote wamejikuta wakiiwania saini yake kwa ajili ya msimu ujao.

Kabunda ambaye jina lake lilitajwa sana dirisha la usajili baada ya Wekundu wa Msimbazi hao ambao walikuwa na uhakika wa kumsajili kwa vile kocha wa wakati huo wa Mwadui ambaye ni mwanachama wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, aliwahakikishia kwa mbwembwe zote kwamba atafanikisha lakini ghafla akaanguka miaka miwili kwenye klabu hiyo ya Shinyanga.

Lakini sasa Wekundu hao wa Msimbazi wameanza upya mbio hizo za kuwania saini hiyo, lakini si peke yao ambapo sasa vita imeingiliwa pia na matajiri wa Azam ambao nao wanamhitaji kwa msimu ujao.

Chanzo makini kutoka ndani ya klabu hizo zimelieleza gazeti hili kwamba, uongozi wa timu hizo unafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanapata saini ya winga huyo kwa ajili ya msimu ujao.

“Katika suala la usajili kwa sasa hasa wachezaji wa ndani linafanywa kimya kimya, kwa kufuata mapendekezo ya benchi la ufundi ambapo anahitaji wapi kurekebishwe,” alisema.

Lakini BINGWA lilimtafuta Katibu Mkuu wa Mwadui FC, Ramadhani Kalao, kuhusiana na kuhitajika kwa mchezaji huyo, ambapo alisema kwa sasa amebakiza mkataba wa miezi sita na mchezaji huyo ambaye tayari wameshaanza mazungumzo kuhusu mkataba mpya.

“Si Simba na Azam tu hata African Lyon nao wanaonekana kumhitaji ila nasi pia bado ni mchezaji wetu na tayari tumeanza mazungumzo ya awali ya kumpa mkataba mpya,” alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*