JUNI CALAFAT ‘ASKARI’ WA PEREZ ANAYEWINDA KIMYA KIMYA

 

NA MARKUS MPANGALA

RAFIKI yangu mmoja alinitumia picha ya mchezaji aliyevaa jezi yenye rangi ya njano, bluu na ufito mweupe kupitia mtandao wa WhatsApp. Baada ya kutuma picha hiyo akaandika maneno yafuatayo: “Babu yenu kaanza kusajili wajukuu zake, nani atawalea akiondoka.”

Baada ya kuandika ujumbe huo akaongezea na emoji za kucheka na utani. Nilielewa mara moja kuwa picha niliyotumiwa inamhusu mchezaji anayetakiwa au amesajiliwa Madrid kwa sababu sikuwa na taarifa zake.

Ikabidi nimuulize huyu mtoto aliyenitumia ni nani. Kwa staha na madoido akanijibu ndiye mchezaji mpya wa Madrid, lakini ana miaka 17 tu, anaitwa Alan de Souza Guimaraes, kutoka klabu ya Palmeiras ya Brazili.

Nikaongeza swali kwake ni sababu gani inamfanya kukebehi usajili wa kijana huyo? Jawabu lake lilikuwa rahisi tu, kwamba Florentino Perez ameanza kusajili wachezaji wadogo badala ya Galacticos.

Mimi ni shabiki wa Real Madrid na ndio maana kolamu hii iliitwa ‘Madridista’ kwa miaka mitatu sasa. Kwa kwakuwa ninakuwa na taarifa nyingi sana kuhusiana na timu hiyo, basi wengine wanatumia kunikebehi. Lakini ndiyo soka lilivyo, utani na uchokozi ni kawaida.

Kwa faida ya wasomaji wa safu hii nimeleta utani wa rafiki yangu huyo kwa sababu maalumu. Kwangu mimi usajili wa Alan de Souza ni jambo la kawaida na kwa hakika napongeza usajili huo. Ninazo sababu kama tatu hivi za kueleza kwanini ninapongeza.

Anza hivi!                            

Kuna sera inayotekelezwa na Florentino Perez ambayo inajieleza bayana kwa sasa. Sera hiyo ilianza wakati ambao Zinedine Zidane akiwa Mshauri wa michezo wa Rais wa Real Madrid ambapo walitaka kuhakikisha wachezaji wanasajili vipaji kutoka Hispania.

Perez mwenyewe anaiita “Made in Spain.” Ndiyo maana unaona kikosi cha Real Madrid kina vipaji vingi vya Kihispania, Isco, Marco Asensio, Dani Ceballos na Jesus Vallejo. Pia bila kumsahau kiungo mkabaji wetu wa zamani, Asier Illarramendi ambaye ameuzwa alikotoka (Real Sociedad) kwa sababu maisha ya Madrid yalikuwa magumu kwake.

Ninamuunga mkono kwa sera kwa sababu kwanza inalinda vipaji vya Kihispania vyenye uwezo wa kuichezea Real Madrid na pili amefanya hivyo kama kujibu mapigo ya Barcelona ambao walikuwa na kikosi kizuri kwa misimu kadhaa wakiwa na muunganiko kutoka La Masia.

Perez amefanya uamuzi mgumu ambao lengo lake ilikuwa kushindana na rekodi za Pep Guardiola aliyekuwa kocha Barcelona. Kwa Wakalunya wanajisifu sana kwa rekodi za Pep, naye Perez akaamua kumpa kazi Zinedine Zidane.

Tukumbushane kuwa Zidane alikuwa mafunzoni katika klabu hiyo ikitarajiwa siku za usoni awe kiongozi hapo. Lakini alibadili mawazo siku za mwisho za kumaliza mafunzo yake na kuwaambia Perez kuwa anataka kuwa kocha si kiongozi wa aina yoyote pale Madrid.

Katika nafasi hiyo sasa ya kupatiwa mafunzo yupo Raul Gonzalez. Naye anapitia njia zilezile alizopita Zidane kwa nia ya kumfanya kuwa kiongozi ajaye klabuni. Zidane amepata mafanikio makubwa akiwa kocha kama alivyokuwa mchezaji. Sasa hivi mjadala unakuwa kulinganisha rekodi za Zidane na Pep Guardiola. Hilo limekwisha.

Juni Calafat

Niliwahi kuandika kuhusu huyu mtu katika safu hii. Nilielezea kuwa yeye ni miongoni mwa watu wanaotengeneza Real Madrid ijayo. Mwaka 2014 aliajiriwa na klabu ya Real Madrid. Calafat ni raia wa Brazil. Wengi hawalijui jina hili. Inawezekana hata baadhi ya mashabiki wenzangu ambao hawajui kuwa kazi ya huyo jamaa ni ipi. Lakini tutaelekezana.

Juni Calafat ni bosi wa kusaka vipaji nje ya Hispania kwa ajili ya Real Madrid hususani kanda ya Amerika Kusini. Kazi yake ni kuzurura katika nchi za Brazil, Argentina, Uruguay, Chile, Peru, Colombia na nyinginezo za bara hilo. Yeye anachokitaka ni kufukuzia vipaji ambavyo vinakuja kusajiliwa Madrid. Ndiyo maana sijashangaa kusajiliwa Alan de Souza.

Kwahiyo rafiki yangu na wale watani zetu watambue kuna mtu wa shughuli anazunguka huko na huku kusaka vipaji mapema kabla havijaonekana kwingine.

Chini ya hekaheka za Calafat ndiyo tumesikia majina ya Alan de Souza ambaye amenunuliwa kwa euro milioni 3.5 tu. Majina mengine tuliyosikia ni Vinicius Junior mwenye miaka 17 kutoka klabu ya Flamengo ya Brazil. Kipaji cha Vinicius Junior kimesababisha Real Madrid kumwaga noti za uhakika kiasi cha euro milioni 45.

Calafat amehusika katika usajili wa makinda, Lucas Silva, Martin Odegaard (Norway) na Wabrazil wafuatao; Douglas Abner, Augusto, Pablo Felipe na William Jose, wakati Fede Valverde ni raia wa Uruguay. Na hapo hapo unamsahau vipi mshambuliaji hatari na galactic wa Castilla, Sergio Diaz? Wote hao wamejiunga na akademi ya Castilla. Tayari anamtolea macho kinda mwingine mpya Lincoln. Siku ukisikia Lincoln amejiunga Real Madrid basi ujue ni kazi ya Calafat. Hilo limekwisha.

Calafat ndiye askari wa Florentino Perez ambaye yuko mawindoni kimya kimya anaisuka Real Madrid ijayo. Alan De Souza anaelekea katika akademi yetu ya Castilla. Huko ataungana na Sergio Diaz na vijana wenzake wanaopikwa na Santiago Solari kabla ya kujiunga timu ya wakubwa.

Mkasa wa Ricardo Kaka

Kuna mkasa huu ambao Perez hatakiwi kuusikia. Miaka ya nyuma wakati Jorge Valdano akiwa mtendaji wa Real Madrid aliwahi kupendekeza jina la Ricardo Kaka asajiliwe. Lakini Perez alikataa kabisa akasema hana mpango wa kusajili kijana huyo. Akaongezea kuwa anataka kumsajili mchezaji ambaye ataongeza mauzo ya jezi klabuni na kuboresha mambo ya masoko si kwenda kuanza maisha. Perez alisema Kaka aende klabu nyingine lakini watamsajili akiwa mchezaji ghali zaidi kwa fedha zozote lakini si kipindi alichokuwa kinda.

Majibu hayo yalishuhudia Kaka akielekea AC Milan. Umahiri alioonyesha kule AC Milan sote tunaujua. Perez aliapoamua kumnunua Kaka, alikuwa amechelewa sana. Makosa yake yalisababisha Kaka asiwe mchezaji wa Madrid. Alipomnunua ilikuwa kama wasemavyo Waingereza, “Too late”.

Previous Article
Next Article

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*