JPM, Kenyatta wataniana 3-2 za Afcon

MWANDISHI WETU, CHATO

RAIS Dkt. John Magufuli na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, waliwaacha wananchi wa Chato, mkoani Geita na vicheko walipokumbushia matokeo ya michuano ya Kombe la Afrika inayoendelea Misri ambapo Harambee Stars iliifunga Taifa Stars 3-2.

Rais Kenyatta yupo nchini kwa ziara ya siku mbili kwa mwaliko maalumu wa Rais Magufuli na aliwasili jana mchana katika Uwanja wa Ndege wa Chato.

Akizungumzia kuhusu mechi hiyo, Rais Kenyatta alisema mechi kama hizo, zinazohusu majirani, zinadumisha uhusiano, ukiachia mbali matokeo ya uwanjani.

“Tumechapana kule Cairo, Misri. Kila mtu na timu yake, Harambee Stars na Taifa Stars nafikiri siku hiyo hakuna mtu aliyelala. Lakini hiyo ndiyo hali ya michezo, tulishindana na safari hii Kenya ikaipiga Taifa Stars. Kwa upande mwingine, timu yenu ilikuwa nzuri mlipocheza na Senegal kwasababu mlifungwa mbili, wakati sisi tulifungwa tatu,” alisema Rais Kenyatta.

Alizishauri timu zote mbili zipambane ili wakati mwingine zifike fainali na endapo mojawao atashinda, basi mwingine pia ni mshindi kwasababu marafiki mambo yao ndivyo yanavyokwenda.

Naye, Rais Magufuli, aliwaacha wananchi kwa vicheko aliposema makubaliano katika mechi hiyo ilikuwa watoke sare ya mabao 2-2, ila amemsamehe Rais Kenyatta kwa Harambee Stars kufunga bao la tatu.

“Uhuru Kenyatta amekuja kuniomba msamaha kwa sababu ametufunga mabao 3-2, kwasababu tulikubaliana tufungane mabao 2-2. Tulipofunga la pili, sisi tukatulia, yeye akaongeza la tatu, kwa hiyo nikasema ngoja nimsubiri atakuja kuomba msamaha,” alisema Rais Magufuli.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*