JKT Tanzania wamweka njiapanda Shime

NA ZAINAB IDDY

KOCHA Mkuu wa JKT Tanzania, Bakari Shime, amesema kitendo cha kusimamishwa na mabosi wake kimemuweka njiapanda, kwani hajui nini hitimisho la adhabu hiyo.

Jumatatu ya wiki iliyopita, uongozi wa JKT Tanzania ulimsimamisha Shime kwa madai ya kutoridhishwa na mwenendo wa kikosi chake Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza na BINGWA jana, Shime alisema amebaki njiapanda kwa kuwa barua aliyopewa haijampa mwongozo atakuwa nje ya timu kwa muda gani.

“Sijui nini hatima ya jambo hili, bora wangeniambia wamenifukuza kazi nikajua moja kuliko kupewa barua ya kunisimamisha kwa muda usiojulikana, huku nikinyimwa nafasi ya kusikilizwa,” alisema Shime.

“Naheshimu mkataba wangu, hivyo inanilazimu kuendelea kusubiri hadi pale watakapoamua kuniita na kunipa nafasi ya kunisikiliza juu ya madai yao.

 “Tangu walipotangaza nimepewa barua ya kusimamishwa napokea simu nyingi za viongozi wa timu nyingine wakitaka nikafanye kazi kwao, lakini nashindwa kwa kuwa bado nina mkataba na JKT Tanzania na haujavunjwa, kwangu hii ni adhabu kubwa,” aliongeza Shime.

Katika msimamo wa ligi, JKT Tanzania inashika nafasi ya tisa, ikiwa imecheza michezo 30 na kujikusanyia pointi 36, huku mechi ya mwisho ambayo inadaiwa kusababisha kusimamishwa kwa Shime wakifungwa mabao 6-1 dhidi ya Azam FC.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*