googleAds

JITU MWITU…Ukisikia Maguire ujue ni furaha tu Man United

MANCHESTER, England

HARRY Maguire. Ndio, kila jina hilo linapotajwa ni furaha miongoni mwa mashabiki wa klabu ya Man United, hata wakongwe nao wanaibuka na kumwagia sifa beki huyo.

Mmoja wa wachezaji wa zamani wa klabu hiyo, mlinda mlango, Peter Schmeichel, amedai kuwa kwa muda mrefu beki huyo alitengenezwa kwa ajili ya kuwa mchezaji wa Manchester United.

Schmeichel alisema, alishaziona dalili za Maguire kuja kuwa mchezaji wa Man Utd tangu akiwa Leicester City, anakocheza mwanae ambaye pia ni mlinda mlango, Kasper.

Kasper alitua Leicester mwaka 2011 na aliweza kucheza sambamba na Maguire katika klabu hiyo kwa muda wa miaka miwili, kabla ya Mwingereza huyo kuhamia Old Trafford kwa kitita cha pauni milioni 80.

“Ngoja niseme hili, nilivutiwa na uwezo wa Maguire tangu nilipomuona kwa mara ya kwanza akicheza.

“Nadhani ni katika mechi kadhaa, nilikuwa nikipata fikra kwamba ‘huyu ni mchezaji anayefaa kucheza Manchester United’. Ni mchezaji imara.

“Bila shaka kila mtu anakumbuka namna alivyocheza kwenye fainali za Kombe la Dunia, kila mechi alikuwepo na alienda sawa na presha ya michuano. Alikuwa ni mmoja wa wachezaji bora wa timu ya England.

“Ni beki, lakini mtazame anavyoukokota mpira kwa kujiamini. Ni mabeki wa kati wachache mno wenye ubora huo. Wengine wanadhani hana mwonekano usioridhisha, lakini naamini atafanya vizuri akiwa Man Utd,” alisema Schmeichel.

Aidha, mkongwe huyo wa zamani alikiri wazi kwamba beki huyo ataituliza vyema safu ya ulinzi ya Man Utd kutokana na utulivu alionao akiwa dimbani.

Maguire alianza maisha yake mapya Old Trafford kwa kuzikonga nyoyo za mashabiki wa Man Utd kwa kuisaidia kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Chelsea.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*