googleAds

Jeuri mpya ya Simba hii hapa

Winifrida Mtoi

SIMBA wanastahili kutembea vifua mbele kutokana na kile kinachoendelea ndani ya kikosi chao, huku jeuri yao kubwa ikiwa ni moja tu, ubora wa safu yao ya kiungo yenye mafundi wanaojua kuuchezea mpira, lakini pia kufunga mabao.

Licha ya baadhi ya wachezaji kuwa majeruhi, Simba bado wana jeuri ya kuendelea kutamba katika mechi zao na kufunga mabao mengi bila kujali nani amesimama mbele.

Wekundu wa Msimbazi hao, kwa sasa wana uhakika wa kupata mabao bila hata ya uwepo wa washambuliaji wao mahiri wa kati, Meddie Kagere au John Bocco kutokana na kuimarika kila idara.

Kipindi cha nyuma ilikuwa ni shida Wanamsimbazi hao kufunga mabao endapo uwanjani watawakosa washambuliaji wao tegemeo, tangu enzi za Emmanuel Okwi, hadi sasa Kagere na Bocco.

Mechi nne za karibuni za Simba, zimedhihirisha kuwa kocha wao, Sven Vandenbroeck, ameamua kutengeneza umoja kama  nyuki na kuwapa kazi kubwa mabeki wa timu wanazokutana nazo.

Ukiangalia katika michezo ya hivi karibuni, wakati mabeki wa timu pinzani wakihangaika kumzuia Kagere, wamekuwa wakishtukia nyavu zao zikitikisika kutokana na shuti lililopigwa kutoka katikati ya uwanja.

Katika mechi nne Simba ilizoshinda, mabao mengi yamefungwa na viungo, hali inayoifanya timu hiyo kuonekana ya tofauti na nyingine zinazotegemea zaidi washambuliaji.

Ukiangalia kati ya mabao 35 yaliyofungwa na Simba katika mechi ilizocheza, 20 yamewekwa kimiani na viungo, huku mengine wakichangia mawinga, mabeki na washabuliaji, wakati Kagere akifunga 11.

Viungo ambao wameonekana kuja juu, wakichuana kufunga mabao ni Clatous Chama na Francis Kahata wanaongoza wakiwa wamefunga mabao matano kila mmoja.

Pia, wapo Hassan Dilunga mwenye mabao manne, Sharaf Shiboub (3), Jonas Mkude (2) na Ibrahim Ajib moja.

Tofauti na kutupia nyavuni, viungo hao wamekuwa chachu ya kuzalisha mabao yaliyofungwa na wengine, Shiboub na Ajib wakiongoza wakiwa na ‘assists’ tano kila mmoja, Chama na Kahata tatu, Dilunga mbili na Mkude moja.

Kitendo hicho kimemfanya Sven kujiamini kupata matokeo wakati wowote na kumpa wigo mpana katika upangaji wa kikosi chake.

Sven alizungumzia mwenendo wa timu yake hiyo akisema anaridhishwa na viwango vya nyota wake japo kuna upungufu hasa eneo la mbele katika kutumia nafasi zinazotengenezwa.

“Unapocheza mechi kikubwa kwanza ni matokeo bila kujali nani amefunga, napenda ushirikiano wa wachezaji wangu, kitu nitakachofanya ni kutafuta suluhisho la matumizi mazuri ya pasi,” alisema Sven.

Katika msimamo wa ligi hiyo, Simba inaongoza ikiwa na pointi 41, ikicheza mechi 16, ikishinda 13, sare mbili na kupoteza moja.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*