googleAds

JESHI LA SIMBA VITANI

NA WINFRIDA MTOI

JESHI la mabingwa watetezi Ligi Kuu Bara, Simba, ni kama halijaridhika na kile kilichovuna katika michezo minne iliyopita licha ya kukusanya pointi zote 12.

Sasa kikosi hicho kinataka kuonyesha kuwa bado kinataka kuweka historia ya kipekee katika soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla, kutokana na inavyohaha kuhakikisha inafanya mambo makubwa zaidi.

Malengo makubwa ya Wekundu wa Msimbazi ni kutetea ubingwa ili kurejea katika michuano ya kimataifa, hivyo mkakati uliopo ni kuzivuruga timu zote za Bara kwa kutoa vichapo.

Licha ya mkakati huo, uongozi umekuwa mkali kuhakikisha kunakwepo na nidhamu lengo likiwa ni kuinua hadhi ya klabu hiyo kongwe.

Simba ilianza mbio za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu kwa kuzinyamazisha timu sumbufu mbili za Mtibwa Sugar ambao waliichapa mabao 2-1, kisha kuwafunga Kagera Sugar 3-0 ugenini.

Katika mechi nyingine walizocheza, Simba waliwafunga JKT Tanzania mabao 3-1 na Biashara United 2-0.

Kama vile haitoshi Simba sasa wameamua kuelekeza nguvu zao katika mechi yao dhidi ya Azam FC inayotarajiwa kupigwa baadaye mwezi huu kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu itachezwa Oktoba 23 mwaka huu, lakini kabla ya mechi hiyo Simba inatarajia kucheza michezo mitatu za kirafiki wakianza na Bandari FC ya Kenya inayonolewa na straika wa zamani wa Yanga, Ben Mwalala, Jumamosi hii katika Uwanja wa Uhuru.

Baada ya mechi hiyo, Wekundu hao wa Msimbazi watasafiri kuelekea Kigoma kucheza dhidi ya Mashujaa FC Oktoba 14 ambayo ni Siku ya Nyerere kabla ya kukipiga na mabingwa wa Burundi, Eagle Noir, siku mbili baadaye, michezo yote ikichezwa katika dimba la Tanganyika, mjini Kigoma.

Akizungumza na DIMBA Jumatano, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema wameamua kucheza michezo ya kimataifa ili kupata kipimo sahihi kulingana na mahitaji ya timu yao.

Alisema kwa aina ya wachezaji walionao, tathimini nzuri ni kucheza mechi ya kimataifa zenye uwezo unaolingana na timu yao ili kiwe kipimo cha uhakika.

“Kipimo cha Simba kama ipo katika mapumziko, ni mechi za kimataifa na ndiyo lengo la kwenda Kigoma kuifuata Eagle Noir ya Burundi, lakini Mashujaa tutacheza nao kwa sababu ni wenyeji wetu,” alisema meneja wa Simba.

Rweyemamu alieleza kuwa michezo hiyo itawajenga vizuri wachezaji wao wasiokuwepo katika timu za taifa ili wenzao watakaporejea wawakute wakiwa fiti zaidi.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*