HUYO MAKAMBO ACHA KABISA

*Apiga bao matata mbele ya ‘msitu’ Moro

*Tshishimbi mnayemjua amerudi, Ngassa acharuka

NA MICHAEL MAURUS


MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga, Heritier Makambo, ameonyesha kuwa ni moto wa kuotea mbali katika suala zima la kucheka na nyavu, baada ya jana kufunga bao ‘bab kubwa’ huku akiwa amebanwa na mabeki watatu.

Katika mazoezi ya Yanga yaliyofanyika jana asubuhi kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini hapa, wachezaji wote wa timu hiyo walionekana kuwa makini mno kuonyesha jinsi walivyopania kuwafariji mashabiki wao.

Mazoezi hayo yalianza saa mbili kwa programu ya kusaka pumzi, kabla ya wachezaji kupewa maelekezo ya kiufundi na baadaye kuyafanyia kazi uwanjani.

Kila mchezaji alionekana kufanya mazoezi kwa bidii tofauti na baadhi ya wapenzi wa Yanga wanavyoamini kuwa morali ya vijana wao imeshuka.

Na kwa jinsi walivyoonyesha katika mazoezi hayo ya jana, iwapo wataendelea kuwepo kambini mjini hapa na kupewa sapoti ya nguvu na mashabiki wao, ligi itakapoanza watakuwa wameiva balaa.

Kwa muda wote waliokuwa wakicheza walionekana kutegeana, lakini baada ya makocha kugawa vikosi viwili hakuna aliyeonekana kutegea mazoezi, kila mmoja alikuwa akihaha kutafuta mpira pale ulipokuwa kwa mpinzani lakini pia kufunga ili kupewa pasi.

Makambo ambaye bado mashabiki wa Yanga hawajamfaidi, ameonyesha si wa kubeza kwani ana nguvu, mbio na shabaha.

Kubwa zaidi, ni mpambanaji asiyekubali kushindwa kirahisi kama ilivyokuwa kwa baadhi ya straika wa Yanga msimu uliopita, ambao wakipoteza mpira huishia kushika viuno na kusubiri kutafutiwa na wenzao kiasi cha kuigharimu timu.

Moja ya bao alilofunga lilikuwa la aina yake kwani baada ya kuupokea mpira, alijikuta amekabwa na mabeki watatu wakiongozwa na Shaibu Abdallah ‘Ninja’, lakini aliwazidi ujanja na kumfunga kipa mpya, Nkizi Kindoki Klaus, wakiwa wamembana kitendo kilichomsababishia kuumia.

Kwa upande wake, kiungo Pappy Tshishimbi, ameonekana ‘kuzaliwa upya’, kwani alikuwa akihaha vilivyo muda wote wa mazoezi hayo akipiga mapande yale ya hatari kama ilivyokuwa siku zake za mwanzoni Jangwani.

Mbali ya kupiga pasi murua, Tshishimbi wa jana alikuwa akihaha kila kona kusaka mpira au kutafuta wa kumpa pasi kuonyesha jinsi alivyopania kuuwasha moto msimu huu.

Naye kipenzi cha Wana-Yanga, Mrisho Ngassa, anaonekana kupania kufanya vizuri ndani ya kikosi hicho kuwafuta machozi mashabiki wa timu hiyo kutokana na jinsi alivyokuwa akihaha uwanjani kama ilivyokuwa kwa Deus Kaseke, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mohammed Issa ‘Mo Banka’ na wengineo.

Kwa upande wa kipa, Nkizi, hadi jana bado ilikuwa vigumu kwa BINGWA kumpima uwezo wake, kwani hakuwa akipata kashkash kutokana na uimara wa mabeki wake.

Kwa ujumla kambi ya Yanga mjini hapa inaendelea vizuri kama alivyothibitisha mratibu wa timu hiyo, Hafidh Salehe, alipozungumza na BINGWA.

“Kambi yetu inaendelea vizuri tunamshukuru Mungu, kama ulivyoona vijana wanapambana hasa mazoezini kujiandaa na mechi zetu zijazo,” alisema Saleh.

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*