HIYO MADRID YA CONTE TUMWACHIE MUNGU

MADRID, Hispania


HAKUNA asiyejua kuwa Real Madrid imeuanza vibaya msimu huu na kichapo cha mabao 5-1 walichokipata juzi kutoka kwa mahasimu wao, Barcelona, kimethibitisha hilo.

Kupoteza mchezo huo kulikiweka hatarini kibarua cha kocha Julen Lopetegui, ambaye ni miezi michache tu imepita tangu alipomrithi Zinedine Zidane ‘Zizou’.

Jana ilielezwa kuwa Lopetegui angetimuliwa baada ya Rais wa Madrid, Florentino Perez, kukutana mezani na wakurugenzi wake kujadili mustakabali wa mchezaji wao huyo wa zamani.

Jina la Antonio Conte ndilo linalozungumziwa zaidi jijini Madrid, hasa baada ya kuonekana haitakuwa rahisi kuinasa huduma ya kocha wa Tottenham, Mauricio Pochettino.

Taarifa zilidai kuwa Lopetegui atamwachia majukumu kocha wake msaidizi, Santiago Solari, kabla ya Conte kuanza kazi rasmi wiki ijayo.

Hata hivyo, wachambuzi wa soka barani Ulaya wanaamini Conte atakifanyia marekebisho makubwa kikosi hicho, wakisema si kipana.

Je, ni mastaa gani wanaotarajiwa kutua Santiago Bernabeu pindi Conte atakapokabidhiwa rasmi mikoba ya kuliongoza benchi la ufundi la Madrid?

Mauro Icardi

Hakuna ubishi kuwa Madrid wanahitaji saini ya straika atakayeweza kuchukua nafasi ya Karim Benzema aliyeshindwa kulitendea haki eneo la ushambuliaji.

Conte anatajwa kuwa mmoja kati ya mashabiki wa Icardi raia wa Argentina. Kocha huyo anamjua vizuri Icardi kwa kuwa alifanya naye kazi Italia akiinoa Juve na timu ya taifa hilo.

Marcos Alonso

Licha ya kwamba ni siku chache tu zimepita tangu aliposaini mkataba mpya, hiyo haimaanishi kuwa Mhispania huyo hawezi kubebwa na Madrid hasa ikiwa Conte atamhitaji.

Itakumbukwa kuwa Alonso alikuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Conte na hata kung’ara kwake kulitokana na kuaminiwa na kocha huyo.

Uzuri ni kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27, ni mzaliwa wa jijini Madrid, hivyo usajili huo ni kama kurudi nyumbani.

Pia, kipaji chake kiliibuliwa na ‘academy’ ya Madrid mwaka 2008 ingawa baadaye aliingia mara moja tu katika kikosi cha wakubwa.

Kwa muda mrefu sasa, Alonso anayecheza nafasi ya beki wa kushoto amekuwa akihusishwa na mpango wa kwenda  Juventus lakini kama Conte atampigia simu, ni wazi atavutiwa zaidi kwenda Bernabeu.

Neymar

Historia ya Madrid na saini ya Neymar haikuanza leo, ni kwa miaka mingi wamekuwa wakitamani kuwa na huduma yake kikosini.

Sehemu kubwa ya mabosi wa klabu hiyo akiwamo Rais Florentino Perez, wanaamini kuwa Mbrazil huyo ndiye mrithi sahihi wa Cristiano Ronaldo aliyewakimbia na kwenda kujiunga na Juve.

Habari njema kwa mashabiki wa Madrid ni taarifa zilizoibuka hivi karibuni, zikidai kuwa hata mchezaji huyo anataka kurejea Hispania alikowahi kuichezea Barcelona.

Kwa upande wa Neymar, licha ya kuripotiwa kutakiwa tena Barca, kuna uwezekano mkubwa wa kuvutiwa na dili la Madrid, kwa kuwa huko anakwenda kuziba pengo la Ronaldo, mmoja kati ya wanasoka bora duniani.

Hata hivyo, kuinasa saini yake ni wazi Madrid watalazimika kuvunja kibubu, kwamba lazima kiasi cha fedha watakachokitumia kivunje rekodi ya usajili katika ulimwengu wa soka.

Eden Hazard

Kama ilivyo kwa Alonso, ushawishi anaoweza kuwa nao Conte kwa Hazard una faida kubwa kwa Madrid kufanikiwa kumsajili Mbelgiji huyo.

Conte na Hazard walikuwa pamoja pale Chelsea, hivyo haitakuwa kazi ngumu kwa Madrid kuwaunganisha tena wawili hao nje ya Stamford Bridge.

Kwa miaka yao miwili pale Chelsea, waliwahi kutajwa kuwa na uhusiano mbovu, jambo ambalo kila mmoja hasa Hazard, alilipinga vikali akisema ni uzushi mtupu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*