HISTORIA YA BONGO STAR SEARCH

NA MWANDISHI WETU


 

HATIMAYE Shindano la Kusaka Vipaji la Bongo Star Search (BSS) limerejea tena, baada ya mwaka jana kushindwa kufanyika.

Mkurugenzi wa Benchmark 360 Ltd, Rita Paulsen, alitangaza ujio huo mpya ambao wameshirikiana na Kampuni ya ving’amuzi vya StarTimes, Star Media Ltd na shindano hilo litarushwa kwenye chaneli yao ya StarTimes Swahili.

Paulsen na Meneja wa Masoko wa StarTimes, David Malisa, walisema wamekusudia kuinua vipaji vya vijana kama walivyokuwa wakifanya na kuwaburudisha wateja wa ving’amuzi vyao.

BINGWA limeorodhesha baadhi ya wasanii waliowahi kushinda shindano hilo lenye mashabiki wengi nchini na historia kubwa.

Jumanne Idd

Shindano hilo la BSS kwa mwaka huu litakuwa ni la tisa tangu lililopoanza kufanyika kwa msimu wa kwanza wa mwaka 2006/2007 na Jumanne Iddi kuwa mshindi wa kwanza wa mashindano hayo.

Katika shindano hilo la kwanza mshindi huyo, Jumanne, alipewa zawadi ya gari ambalo lilikadiriwa kuwa na thamani ya shilingi milioni 20.

Misoji Nkwabi

Msimu wa 2007/2008 ilikuwa ni zamu ya wadada kuibuka kidedea baada ya Misoji Nkwabi kuwa mshindi na kupata zaidi ya shilingi milioni 20 pamoja na simu kutoka Kampuni ya LG, masofa kutoka Living Room, runinga, kompyuta.

Paschal Cassian

Paschal Cassian kutoka Mwanza aliibuka mshindi wa Bongo Star Search mwaka 2009, akijinyakulia shilingi milioni 25 na kupata mkataba wa kurekodi albamu kutoka Kampuni ya Benchmark Productions.

Katika fainali hiyo iliyofanyika Diamond Jubilee Hall, jijini Dar es Salaam, wakati wa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Peter Msechu, alifanikiwa kuwa mshindi wa pili na Kelvin Mbati, Jackson George na Beatrice William wakishika nafasi ya nne na tano.

Mariamu Mohamed

Msimu wa nne wa shindano hilo mwaka 2010 mshindi alikuwa Mariam Mohamed ambaye aliimba sana nyimbo za taarabu alijinyakulia shilingi milioni 30.

Nafasi ya pili na tatu alishinda James Martin na Joseph Payne, ambapo walishinda shilingi milioni 10 na 5, huku wanne na watano wakiwa ni Bella Kombo na Salum Waziri ambao walipata shilingi milioni 1.7 katika fainali hizo zilizofanyika Mlimani City.

Haji Ramadhani

Mwaka 2011 ilikuwa ni fursa ya washiriki wengine wa BSS ambao hawakupata nafasi ya kushinda kusaka ushindi katika shindano hilo ambao msimu huo liliitwa ‘Second Chance’ na Haji Ramadhani kujinyakulia shilingi milioni 40 kwa kuibuka mshindi.

Walter Chilambo

Walter Chilambo aliwashinda wapinzani wake wanne katika fainali iliyofanyika mwaka 2012 kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam na kuibuka kidedea.

Walter ambaye alijinyakulia shilingi milioni 50 alishindwa kuhimili furaha ya ushindi na kuanguka chini baada ya kutangazwa na Jaji Mkuu wa BSS, Paulsen, ambaye naye alitokwa na machozi.

Nyota huyo ambaye sasa anatamba kwenye muziki wa Injili, aliwashinda Salama Abushir na Wababa Mtuka, walioshika nafasi ya pili na tatu.

Emmanuel Msuya

Baada ya Walter ikawa zamu ya Emmanuel Msuya kutoka Mwanza aliyejinyakulia shilingi milioni 50 kwa kuwa mshindi wa mwaka 2013, akiwashinda Amina Chibaba, Maina Thadei, Melisa John na Elizabeth Mwakijambile, lakini Amina na Maina walitolewa raundi ya pili ya fainali hiyo iliyofanyika Escape One, Dar es Salaam.

Kayumba Juma

Shindano la BSS la mwisho kufanyika kabla ya lile la mwaka huu lilikuwa ni lile la mwaka 2015, ambalo Kayumba Juma aliibuka kuwa mshindi na kujinyakulia shilingi milioni 50.

Kayumba aliwashinda Nassibu Fonabo na Frida Amani, wakishika nafasi ya pili na ya tatu katika fainali hiyo iliyofanyika kwenye Ukumbi wa King Solomoni, Namanga jijini Dar es Salaam.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*