HII NDIYO SABABU YA KAULI ZAKE ZA KUKERA

couple-fight

UNAWEZA kusema lolote juu ya maneno katika suala zima la mapenzi, ila huwezi kuubatilisha ukweli huu. Maneno ni moja kati ya sehemu muhimu katika ujenzi ama ubomoaji wa mapenzi.

Asilimia kubwa ya maisha yetu yapo mdomoni. Kwanza tunaongea, tunatafakari, kisha tunatenda.

Wapenzi wetu wanahitaji kusikia kauli za furaha za kupendeza vinywani mwetu.

Kwa asilimia fulani maneno yanajenga ama kubomoa mahusiano yetu.  Na sio katika mapenzi tu, maneno yamekuwa sehemu muhimu sana katika maisha yetu.

Hata mtu awe mfanyaji vipi wa vitendo ila pia watu huwa na utegemezi wa asilimia fulani katika maneno yake.

Hata shuleni pia ni hivi hivi. Kwanza, asome darasani, kisha akatende maabara. Hata haya matendo ambayo tunafanya mara nyingi huwa yanazaliwa katika fikra, yanakuzwa katika maneno, baadaye ndiyo huwa tunatenda.
Nimewahi kusikia kauli nyingi juu ya kupinga thamani ya maneno ndani ya mahusiano. Wapo wanaosikika wakisema matendo ndiyo kila kitu, baadhi wanasema maneno si kitu sana katika mapenzi.

Huenda wakawa sahihi  kwa kutumia nusu ya ubongo kutafakari, ila kwa maana kamili hawako sahihi. Kwanza, anaambiwa kisha anayaona yakitendeka, hapa ndiyo huwa mtu anaweza akakuamini.

Sasa wewe fanya tu matendo bila kumfahamisha ni kwanini unafanya hivyo halafu uone. Hata wakati unataka kuwa naye, ulimpa kwanza maneno kisha ukamuahidi matendo mazuri.

Na kwa uzito wa maneno yako ukamfanya awe makini katika matendo yako kuona kama unaweza kuyasimamia. Na matokeo yake leo ni mwaka wa pili tangu aanze kukuita mume.
Hiyo ndiyo nguvu iliyopo katika maneno. Ukitaka kuiona zaidi tupia macho katika raha na vurugu nyingi katika ndoa. Kwanza huwa maneno, kisha ngumi na mateke hufuata.

Kwanza, huwa maneno, baadaye ndiyo safari ya kuelekea SHOWROOM. Ukitaka kumjua anayekuhitaji chunguza tu kauli zake alafu tupia macho matendo yake.

Kama anakuona wa thamani atakupa maneno ya faraja, kisha atamaliza kwa matendo ya raha.
Unafikiri kwanini kila ukigombana na mwezako bila kujali ukubwa wala uzito wa kosa yeye anakimbilia kusema kama vipi tuachane?

Ni kwa sababu hakuna mtu anayeweza kumvumilia asiyempenda. Kuongea kauli hii huwa haimuumizi kwa sababau kwake, wewe ni kero.
Eti kosa kakufanyia wewe na bado anakwambia amua unachotaka. Kwa ambaye anayekupenda hawezi kukwambia hivi, na badala yake atakuomba msamaha tena kwa upole na unyenyekevu.

Ila kwa huyu, siyo hivyo kwa sababu anakuchukulia kawaida sana. Ukiwa naye sawa, ukiondoka pia humpunguzii kitu.

Ndani ya kauli za mwezako kuna ukweli unaotakiwa kuujua. Ikiwa hisia zake zipo kwako, angalia kauli zake zitakavyosababisha tabasamu ha hamu juu yake.
Hawezi kukukwambia kama vipi tuachache, kwa sababu kwake wewe ni lulu isiyopaswa kupotea. Hawezi kusema amua unachotaka kwa kuwa hapendi kukupoteza.

Kwa kila namna akiona kuna dalili ya wewe kukerwa ama kutaka kuchukua maamuzi yasiyo bora katika ustawi wa mapenzi yenu atajitahidi kuremba maneno na kuwa mpole katika kauli zake ili akufanye nawe uwe mpole na mapenzi baina yenu yaendelee kama kawaida.
Kauli ni kioo cha kilichopo ndani ya nafsi. Ndiyo maana mtu anayekuhofia hata kauli zake pia zinaonesha hivyo.

Hivyo ni kwa sababu ya moyoni mara nyingi huonekana kupitia kauli alafu ndiyo matendo. Ndiyo maana anayekupenda kweli, mbali na kukwambia ila pia atafanya yale yanayoonesha upendo juu yako.

Ni kwa sababu ile ile, ya moyoni huwa yanapitia kwanza katika kauli na kudhihiri katika matendo.
Ziangalie kauli za mwenzako, kisha angalia matendo yake, utajua nini namaanisha.

Ikiwa kweli anakupenda basi hata kauli zake zitachora picha hiyo. Hawezi kutamani muachane katika kauli wala matendo yake.
Kakukosea, unalalamika.. badala ya kukuomba msamaha anakwambia shauri yako bwana! Mtu wa aina hii unaamini anakupenda eti kwa sababu anakupa pesa.

 

Huwazi kama anakufanya bidhaa ndiyo maana hajali kukumiza kupitia kauli zake? Huoni kama anadhani unadhiki sana ndiyo maana anakupa pesa ila kauli zake zinanuka?
Kuwa makini na huyo unayemuita Sweetie! Angalia kauli na matendo yake. Angalia namna anavyotaka kuokoa penzi lenu anapohisi kunataka kutokea dhoruba.

Ona kauli zake unapokosea au anapokosea. Kisha tafakari hatima ya mapenzi yenu. Nafasi inanihukumu wapendwa.
ramadhanimasenga@yahoo.com

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*