googleAds

GETRUDE MWITA: HAKUNA WA KUNIUMIZA KICHWA BONGO, NAMTAMANI VIOLA DAVIS

KARIBU msomaji wa Jiachie na Staa Wako, safu inayokupa nafasi ya kuwa karibu na watu maarufu uwapendao kwa kuwauliza maswali mbalimbali. Leo tupo na mwigizaji nyota anayefanya vizuri katika tamthilia na filamu za Kibongo, Getrude Mwita, karibu.

SWALI: Karim Sadick wa Bugando Mwanza, anasema bila shaka una mpenzi, je, huwa anachukulia vipi kazi yako ya uigizaji kipindi unapokuwa kazini na yeye anahitaji ukaribu wako?

Getrude: Bahati nzuri au mbaya sina mpenzi, mpenzi wangu mimi ni kazi ila nikimpata nadhani atanielezea itakuwaje.

SWALI: Aloyce Kalemba wa Mtwara Mjini anauliza ‘scene’ ipi huwa inakupa ugumu wakati unaigiza?

Getrude: Ukiwa mwigizaji hutakiwi kuwa na kitu kigumu au chepesi, kwangu mimi hakuna ‘scene’ iliyowahi wala itakayowahi kuja kunipa ugumu kuigiza.

SWALI: Rehema Eliya wa Kihonda, Morogoro, anauliza kwanini tasnia ya burudani ina mastaa wa kike wachache na je, familia yako ina mchango gani kwenye kazi zako?

Getrude: Familia yangu ni mashabiki zangu, wananipa sapoti sana, wasichana wanakata tamaa mapema, unakuta  mtu akikatishwa tamaa mara moja, mara mbili anaamua kuacha ndiyo maana tunapata wasichana lakini hawadumu iwe kwenye muziki au filamu, wanaogopa, hawajiamini, hawana uthubutu.

SWALI: Nesta Kambo wa Makete anauliza waigizaji gani hapa Bongo wanakuumiza kichwa unatamani uwe kama wao au uwapite?

Getrude: Hakuna mwigizaji anayeniumiza kichwa, sina mwigizaji ninayetaka kuwa kama yeye ila nataka wao wawe kama mimi.

SWALI: Yeremia wa Jet Lumo, Dar es Salaam anauliza ‘role model’ wako ni nani hapa Bongo na nje?

Getrude: Tanzania sina ‘role model’ kwa kweli ila nje ninaye anaitwa  Viola Davis (mwigizaji wa Marekani).

SWALI: Mama Suzan wa Buguruni Sokoni, Dar es Salaam anasema amewahi kusikia kuwa umeokoka, je, unawezaje kufanya kazi za sanaa za kidunia na kumtumikia Mungu kwa wakati mmoja?

Getrude: Ni kweli nimeokoka nampenda sana Yesu, lakini hiyo hainizuii mimi kufanya kazi zangu za sanaa kwa sababu nafanya katika maadili mema, simkosei mtu, simvunjii mtu heshima, kanisani kwangu siwavunjii heshima ni kipaji ambacho yeye mwenyewe Mungu amenipa kwa hiyo lazima nikionyeshe na nikifanyie kazi.

Kuokoka hainizuii mimi kufanya kazi zangu, wokovu tunaouzungumzia sisi ni kumkubali Mungu kuwa kiongozi na mwokozi wa maisha yako, unamweka ndani na si unamwigizia nje, unavaa nguo ndefu halafu kumbe ni mchawi, kuokoka ni vitu vya ndani yako hivyo vitu vya nje ni mwanadamu tu ana hukumu ila Mungu anaangalia moyo.

SWALI: Romeo Mbesanga wa Tanga, anauliza umeonekana zaidi kwenye tamthilia nyingi zaidi kama Huba, Kimya Milele nk, kuliko kwenye filamu, unadhani kwanini imekuwa hivyo pia kwa mtazamo wako kwanini soko la filamu limeshuka?

Getrude: Nimeonekana kwenye tamthilia zaidi kwa sababu wakati nimeanza kuigiza ndiyo kipindi ambacho filamu zinafifia na ndiyo nimeanza kuonekana, kipaji changu hakikuishia hapo, baada ya mfumo wa tamthilia uliporudi ndiyo nikautumia kama hivyo unavyoona.

Filamu kushuka nadhani ni sisi wenyewe waigizaji, maprodyuza tumefanya soko life kwa sababu tulikuwa tunatoa kazi nyingi ambazo hazina ubora, kwa hiyo ni sisi wenyewe waigizaji, maprodyuza, wasambazaji na elimu ndogo imefanya soko liyumbe.

SWALI: Vedasto Mtega wa Dodoma, anauliza lini ulianza kuigiza na ni mwenyeji wa wapi?

Getrude: Mimi ni mzaliwa wa Mkoa wa Mara, ni mtoto wa mwisho katika familia yenye watoto wanne, wazazi wangu wote wameshafariki kwa hiyo nipo na ndugu zangu wengine, safari ya kuigiza nilianzia shule ya msingi mwaka 2004 mpaka leo.

SWALI: Letisia Marwa, ni mwigizaji chipukizi kutoka Bunda, anasema anakupenda sana pia anataka kujua changamoto zipi ulikutana nazo katika safari yako ya sanaa ikakuumiza?

Getrude:  Changamoto ni kama hivyo kuambiwa huwezi kuigiza, maana kwa kipindi ambacho nimeingia kwenye filamu unaambiwa wewe si mzuri, wewe si mweupe pia kutakwa kimapenzi ndiyo changamoto nilizokutana nazo.

SWALI: Nuru Nyagawa wa Mafinga, Iringa anasema yeye ni shabiki yako namba moja, pia anataka kufahamu kama una malengo katika sanaa au unaigiza igiza tu.

Getrude: Sasa hivi nina kazi kubwa nje ya nchi, nina kazi mpya Kenya, Afrika Kusini na hapa Tanzania, kwa hiyo ni Mungu tu anisaidie sababu ndoto zangu ni kuwa mwigizaji wa kimataifa.

Wiki ijayo tutakuwa Dickson Sound ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa Agnes Masogange na mhandisi magari aliyefanikiwa kutengeneza magari asilimia 90 ya mastaa unaowafahamu hapa nchini, tuma swali lako kwake kupitia namba hapo juu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*