HAZARD AWAPA NENO NYOTA WENZAKE CHELSEA

LONDON, England

MSHAMBULIAJI wa klabu ya Chelsea, Eden Hazard, amewataka wenzake kuunganisha nguvu moja na kupambana ili kuifanya timu yao imalize kwenye nafasi nzuri msimu huu.

Mabingwa watetezi hao wa Ligi Kuu England, walijiweka kwenye mazingira magumu wikiendi iliyopita baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na West Ham.

Hazard ambaye kiwango chake katika wiki za hivi karibuni kimeporomoka, aliuambia mtandao rasmi wa Chelsea kuwa: “Msimu huu umekuwa wa hovyo kwetu. Mabao mengi tuliyofungwa yametokana na makosa ya kizembe. Sisi wenyewe hatufungi mabao ya kutosha.”

“Inabidi tupambane pamoja. Tumebakiwa na mechi sita za ligi na tutafanya kila liwezekanalo tumalize msimu huu ndani ya nafasi nne bora,” alisema Hazard.

Wiki moja kabla ya kucheza na West Ham, Chelsea ilipoteza nafasi nzuri ya ushindi dhidi ya Tottenham, ambapo licha ya kuongoza bao moja waliruhusu mabao matatu na kuaibishwa nyumbani kwao.

“Ujue msimu huu tumepoteza mechi nyingi kwa mtindo unaofanana. Nakumbuka dhidi ya Man United, tuliumiliki sana mchezo lakini tukaishia kufungwa sisi.

“Dhidi ya Spurs, hivyo hivyo tulimiliki mchezo hasa kipindi cha kwanza, mwisho tukapoteza. Msimu huu tuna hali mbaya, hatuna budi kukaza kamba,” aliongeza winga huyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*