googleAds

HAYA YALIIPOOZESHA AFCON 2017

LIBREVILLE, Gabon

HATIMAYE fainali za Mataifa Afrika za mwaka huu (Afcon 2017) zilimalizika juzi nchini Gabon.

Cameroon ndio walioibuka kidedea baada ya kuwafunga Misri mabao 2-1 katika mchezo wa fainali.

Hata hivyo, wachambuzi wa soka wametoa maoni yao juu ya mashindano hayo ambayo ni ya 31 tangu kuanzishwa kwake.

Wengi wameonesha kutovutiwa na fainali za mwaka huu wakisema hazikuwa na mvuto uliokuwa ukitarajiwa na idadi kubwa ya mashabiki wa soka.

Mastaa wengi wakubwa wanaokipiga barani Ulaya walishindwa kuziongoza vema timu zao za taifa na kusababisha kupooza kwa mashindano hayo.

Mfano; Pierre Aubameyang, ambaye alikuwa akitolewa jicho na kutajwa sana kabla ya kuanza kwa Afccon, alishindwa kuifanyia lolote Gabon.

Wakiwa na nyota huyo anayeichezea Borussia Dortmund ya Bundesliga, Gabon waliyaaga mashindano hayo katika raundi ya kwanza.

Lakini pia, hali ilikuwa hivyo kwa Riyad Mahrez wa Leicester City ambaye alishindwa kuibeba Algeria.

Kwa upande wao, licha ya kujaza ‘mafaza’ kikosini, Ivory Coast waliishia kuwa wasindikizaji kama ilivyokuwa kwa Togo ambao walikuwa na  Emmanuel Adebayor.

Lakini pia, kukosekana kwa baadhi ya timu vigogo barani Afrika kulipoozesha michuano hiyo.

Mathalani, kutokuwapo kwa wababe wa soka wa Afrika Magharibi, Nigeria. Wachambuzi wa soka wamefananisha tukio hilo na kitendo cha Brazil kutokuwamo kwenye fainali za Kombe la Dunia.

Ni wazi kuwa Nigeria wamekuwa wakitoa upinzani mkubwa katika michuano hiyo ya Afcon na inaposhiriki katika mashindano hayo, huwa ni fursa nzuri ya kibiashara katika soka.

Kuikosa Nigeria katika fainali mbili mfululizo za Afcon ni majanga kwa michuano hiyo.

Mbali na hilo, ubovu wa viwanja ni changamoto nyingine ambayo kwa kiasi kikubwa imezifanya fainali za Afcon mwaka huu kutovutia.

Licha ya ukongwe wa fainali hizo, bado ni ngumu kufanananisha viwanja vinavyotumika na vile vya mashindano ya Ulaya na Amerika Kusini.

Wachambuzi wa soka wanaamini kuwa michuano ya mwaka huu haikuwa na mvuto kwa kuwa viwanja vilivyotumika havikuwaruhusu wachezaji kuonesha ufundi wao.

Ni ngumu kupima uwezo halisi wa kocha au mchezaji kwani ubovu wa viwanja uliwafanya kusaka ushindi zaidi kuliko kutandaza soka la kuvutia.

Siku chache baada ya mashindano kuanza, wachezaji na makocha walipaza sauti kulalamikia ubora wa viwanja.

Viwanja hivyo ni Stade de l’Amitie, Stade de Franceville, Port Gentil na Stade d’Oyem.

Ingawa timu yake haikushiriki, kocha wa Nigeria, Gernot Rohr, alikosoa viwanja hivyo alipokuwa akihojiwa na kituo cha redio cha RFI cha Ufaransa.

“Wachezaji na makocha hawaridhishwi na hali ya viwanja,” alisema kocha huyo raia wa Ujerumani.

Naye nahodha wa Ghana, Asamoah Gyan, alitupa lawama zake kwa Uwanja wa  Port Gentil, akisema ubovu wake ulichangia timu yake kupoteza mchezo wa Kundi D dhidi ya Uganda ambapo walilala bao 1-0.

Wachezaji wengi walikuwa wakiumia wakati fainali hizo zikiendelea. “Uwanja si mzuri kwani una michanga ambayo inaufanya uwe mgumu,” alisema Gyan.

Katika hatua nyingine, michuano ya mwaka huu iliendeleza utamaduni wa kuwa na utitiri wa makocha wa kigeni, jambo ambalo limekuwa likipigiwa kelele miaka mingi.

Mmoja kati ya wanasoka wakongwe wanaokerwa na wingi wa makocha wa kigeni barani Afrika, ni Kalusha Bwalya wa Zambia.

“Lazima makocha wazawa wawezeshwe na kuyabeba mataiafa yao. Waaminiwe na wavumiliwe wanapokuwa kwenye mashindano makubwa,” alisema Bwalya.

Hoja ya wachambuzi ni kwamba, makocha kutoka Ulaya hawawezi kulipeleka kokote soka la Afrika.

Mbali na madudu hayo, michuano ya Afcon ilikuwa na uzuri wake hasa linapokuja suala la matangazo ya televisheni ingawa mahudhurio ya uwanjani yalipungua pale wenyeji Gabon walipotolewa.

Timu ambazo walau ziliyachangamsha mashindano hayo ni pamoja na Senegal, Ghana, Cameroon na Misri.

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*