HAWAKUWA NA CHAO

Hapa ndipo Modric alipowabwaga Messi, Ronaldo Ballon d’Or

 MADRID, Hispania

HATIMAYE usiku wa kuamkia juzi historia iliandikwa baada ya nyota wa Real Madrid, Luka Modric, kutangazwa kuwa mchezaji bora mpya wa mwaka wa dunia na kukabidhiwa tuzo ya Ballon d’Or, akiwabwaga vinara, Lionel Messi  na Cristiano Ronaldo, waliotamba nayo kwa muda wa miaka 10.

Tuzo hiyo ni moja kati ya mafanikio aliyoyapata kwa mwaka ikiwa ni baada ya nyota huyo wa timu ya Taifa ya Croatia hivi karibuni kunyakua tuzo za mchezaji bora wa mwaka wa Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) la kimataifa Fifa.

Hata hivyo, tuzo hii ya Ballon d’Or  ndiyo inayoonekana kilikuwa ni kibarua kikubwa kwake kutokana na kuwa alikuwa akishindana na mastaa waliowahi kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia wakiwamo, Antoine Griezmann, Kylian Mbappe na Raphael Varane, bila kutaja mchuano mwingine kutoka kwa wababe, Lionel Messi  na Cristiano Ronaldo.

Licha ya kukabiliwa na ushindani huo, Modric, aliweza kukomaa hadi mwisho akitumia kiwango chake na mafanikio aliyoyapata ndani ya mwaka huu na huku akisaidiwa na vigezo vingine  hadi kufikia anatangazwa kuwa mchezaji bora wa sayari hii kwa mwaka huu.

Katika makala haya wachambuzi wa masuala ya soka wamejaribu kuchambua mambo manne ambayo yalimfanya staa huyo aibuke mshindi wa tuzo hiyo ya Ballon d’Or.

1.Watu walitaka mabadiliko

 Licha ya Modric kutangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo ya Ballon d’Or kwa mwaka huu, lakini bado kuna mjadala unaoendelea kama ni kweli alistahili kuwafunika Lionel Messi  na  Cristiano Ronaldo na mjadala huo utaendelea kuwapo kwa muda mrefu.

Hata hivyo, staa huyo raia wa Croatia, amekuwa na kiwango  kizuri katika mashindano yote mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na fainali za Kombe la Dunia na mafanikio mengine ambayo ameyapata kwa mwaka huu yanayomfanya astahili kunyakua tuzo hiyo ya Ballon d’Or.

Msimu uliopita, Messi aliumaliza akiwa mfungaji bora wa La Liga na ligi kubwa tano Ulaya  na vile vile aliisaidia  Barcelona kutwaa mataji mawili ya ligi ya ndani na huku  Ronaldo akiwa kinara katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiiongoza Real Madrid kutwaa kwa mara ya tatu mfululizo ubingwa wa michuano hiyo na pia akimaliza akiwa mfungaji bora kwa mara ya sita mfululizo bila kuhesabu mabao 40 aliyoifungia klabu hiyo katika kipindi hicho.

Hata hivyo, bila kuongopa pamoja na mastaa hao kufanya hivyo, Modric alistahili tuzo hiyo ya  Ballon d’Or kwa kiwango na mafanikioa aliyoyapata ndani ya mwaka huu.

Lakini kama utakuwa na kumbukumbu kilichowahi kuwatokea mastaa kama  Xavi na  Iniesta  mwaka  2010, Frank Ribery, mwaka  2013  na mlinda mlango, Manuel Neuer, mwaka  2014, unaweza kubaini kwamba watu walihitaji mkono mwingine  mpya wa kunyanyua tuzo ya  Ballon d’Or na ndio maana wakampigia kura  Modric.

  1. Messi na Ronaldo walichemka nchini Urusi

Sababu nyingine ambayo ilimsaidia  Modric kuondoka na  Ballon d’Or  kwa mwaka huu ukweli ni kwamba nyota wa Barcelona,  Lionel Messi  na mwenzake wa  Juventus,  Cristiano Ronaldo,  walishindwa kung’ara wakiwa na timu zao za taifa katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika mwaka huu nchini Urusi.

Kabla ya mshindi wa mwaka huu kutangazwa vinara hao walikuwa wameshapokezana mara 10 huku kila mmoja akiwa ameibeba mara tano  na wote walikuwa wakipewa nafasi ya kunyakua tena.

Hata hivyo, baada ya kushindwa kutamba kwenye michuano ya fainali za Kombe la Dunia ndicho kilichowapa nafasi nyota wengine kuchomoza na mmoja wao Modric akapata nafasi ya kuwagalagaza.

  3.Fainali za Kombe la Dunia

Pia kabla ya juzi kutangazwa mshindi, Modric alikuwa ameshajijengea mazingira ya kutwaa tuzo hiyo ya  Ballon d’Or  kufuatia mafanikio ambayo aliyapata katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, UEFA msimu uliopita.

Mbali na hilo pia kiwango alichokionesha wakati wa fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika mwaka huu nchini Urusi nayo ilikuwa ni silaha tosha kuwafunika mahasimu wake.

Akiwa ametwishwa jukumu la unahodha, staa huyo aliweza kufunga mabao mawili muhimu na kutoa ‘asisti’ moja  yaliyoisaidia timu yake kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo kutinga hatua ya fainali.

  1. Kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya

Kuna vitu vingi ambavyo vilimsaidia  Modric katika safari yake ya kutwaa tuzo hiyo ya  Ballon d’Or  kwa mwaka huu na mojawapo ni ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Msimu uliopita Modric alikuwa hakamatiki katika safu ya kiungo akiwaunganisha mabeki na washambuliaji, kutuliza kasi ya mchezo, kutoa pasi murua sambamba na kuimarisha kiwango cha uchezaji kwa timu yake.

Raia huyo wa  Croatia aliumaliza msimu huo akiwa mmoja kati ya wachezaji walioonesha kiwango cha hali ya juu kilichoiwezesha Real Madrid kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo mara tatu mfululizo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*