HAWA HAPA

MADRID, Hispania

KILA kukicha mambo yalionekana kwenda ndivyo sivyo kwa kocha wa Real Madrid, Julien Lopetegui, ambaye alirithi mikoba ya Zinedine Zidane aliyeikacha msimu uliopita baada ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya tatu mfululizo.

Lakini tangu Lopetegui atangazwe kuwa kocha wa timu hiyo yenye mataji mengi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, wameshindwa kufanya vizuri kama vile ilivyotegemewa na mashabiki wa klabu hiyo.

Katika michezo saba waliyocheza hivi karibuni chini ya Lopetegui, Real Madrid hawakufanikiwa kushinda mchezo hata mmoja, yaani walifungwa mitano, sare moja na kushinda mmoja.

Walifungwa mabao 3-0 na Sevilla, kisha wakatoa suluhu na Atletico Madrid, CSKA Moscow waliwapiga bao 1-0 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku Alaves wakiweka pointi tatu mfukoni kwa kuichapa bao 1-0 kabla ya kukubali kipigo kingine cha mabao 2-1 kutoka kwa Levante.

Upande mwingine walifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Viktoria Plzen katika Ligi ya Mabingwa baadaye wakipokea kipigo kikali cha mabao 5-1 kutoka kwa Barcelona.

Baada ya kichapo hicho, hali ya Real Madrid ilionekana kuwa mbaya zaidi na kuepelekea Lopetegui kufukuzwa na mikoba yake kupewa Santiago Solari aliyekuwa kocha wa kikosi cha vijana maarufu kama Castilla.

Katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Melilla kwenye Kombe la Copa del Rey, aliiwezesha Real Madrid kupata ushindi wa mabao 4-0 na kurudisha imani kwa mashabiki wa kikosi hicho cha mabingwa wa Ulaya.

Lakini inaaminika Real Madrid hivi sasa wapo mbioni kutafuta kocha mwingine atakayeziba nafasi hiyo ambayo yupo Solari kwa muda.

Makala haya yanakuletea makocha watatu ambao wanapewa nafasi kubwa ya kurithi mikoba ya Lopetegui ambaye aliwahi kukinoa kikosi cha timu ya Taifa ya Hispania.

MAURICIO POCHETTINO

Pochettino ni kocha ambaye Real Madrid walimtolea macho na kumfuatilia kabla ya kuongeza mkataba wa kuendelea kuitumikia Tottenham kwa muda mrefu zaidi.

Kocha huyo mwenye miaka 46, alifuatiliwa kwa ukaribu zaidi na vigogo wa Real Madrid ambao walikuwa tayari kumkabidhi mikoba ya Zidane, lakini kwa mambo yanayoendelea ndani ya timu hiyo wanaweza kumrudia kwa mara nyingine.

Bado hajafanikiwa kushinda taji lolote akiwa na timu yake lakini amekuwa mmoja wa makocha bora Ulaya kwa sasa kutokana na kile anachokifanya Tottenham.

Kama kweli Real Madrid wanahitaji saini ya kocha huyo itabidi wavunje mkataba wake aliosaini na Tottenham mwanzoni mwa msimu huu ambao unatarajiwa kumalizika mwaka 2023.

Huku ikitambuliwa kuwa katika mkataba huo kuna kipengele cha kumruhusu kuondoka kama kuna timu ikimhitaji.

Kwa hali inavyoendelea ndani ya Real Madrid, kuna uwezekano wakahitaji saini ya kocha huyo wa zamani wa Espanyol na Southampton.

ARSENE WENGER

Wenger hivi sasa yupo nje ya soka baada ya kuondoka Arsenal aliyoitumikia kwa miaka 22 na kuwapa mafanikio kadhaa kwa kipindi chote alichokuwa na kikosi hicho.

Wiki kadhaa zimepita tangu Wenger alipotoboa siri kuwa Januari mwakani atarejea kufundisha tena soka, lakini alishindwa kuweka wazi ni timu gani ataifundisha.

Lakini kwa hali inayoendelea pale Santiago Bernabeu, inaweza kuwafanya kumfikiria kocha huyo wa zamani wa Arsenal na Monaco huku ikikumbukwa miaka ya nyuma aliwahi kupokea ofa ya kuifundisha Real Madrid.

Wenger alikataa ofa zote za Real Madrid na kuamua kubaki na Arsenal, kwa umri wake wa miaka 69 ni kocha mzoefu mwenye kujua kipi cha kufanya huku akisifika kwa kutumia bajeti ndogo ya usajili.

ANTONIO CONTE          

Baada ya kuvuna mafanikio akiwa na Chelsea hivi karibuni, Antonio Conte, ameingia kwenye orodha ya makocha wanaohitajika na Real Madrid kama wakimtimua Lopetegui wa sasa.

Alifanikiwa kutwaa taji la Ligi Kuu England na Kombe la FA kwa misimu miwili aliyokuwa na kikosi cha Chelsea, huku akifahamika zaidi alipowapa Juventus mataji matatu ya Ligi Kuu Italia na Copa Italia.

Lakini taarifa zilizopo zinadai kuwa Real Mdrid wameshindwa kufikia kwenye makubaliano na Conte ambaye alitajwa sana na vyombo vya habari Ulaya kuchukua nafasi hiyo.

 

 

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*