HATUONI DALILI YA KUPATA MEDALI JUMUIYA YA MADOLA

TANZANIA ni moja ya nchi ambazo zitapeleka wanamichezo katika michuano ya Jumaiya ya Madola itakayofanyika  Aprili mwaka huu Mji wa Gold Coast nchini Australia.

Katika michuano hiyo, Tanzania itawakilishwa na timu tano  za michezo ya  riadha, kuogelea, mpira wa  meza, ngumi na paralimpiki huku dalili za kufanya vizuri na kupata medali zikionyesha kutowepo kutokana na maandalizi hafifu.

Matumaini kwa Tanzania  kurejea na medali kama nchi za wenzetu  wanavyofanya vizuri katika michuano hiyo, tunaiona ni ndogo kutokana na timu zitakazoshiriki  kuonekana kusuasua katika maandalizi yake.

Tumeanza kupata wasiwasi  kwa wanamichezo wetu kuweza kufanya vema na baadaye kurejea na medali nchini kwa kuwa hawaonyeshi jitihada za  kushindana na wenzao watakapokuwa Gold Coast.

Tunasema kwamba kwa muda uliobaki kufikia michuano hiyo, tunauona ni mdogo kwa wanamichezo wetu kuweza kufanya maandalizi kwa kiwango cha kuchuana na mataifa mengine.

Mpaka sasa ni timu moja ya meza ambayo imeanza kambi nchini China kupitia mpango wa diplomasia ya michezo, lakini nyingine hazifahamiki zitaanza lini kuweka kambi ya pamoja.

Kama tulivyosema mwenendo tunaouona wa maandalizi kwa wanamichezo wetu  unatutia shaka kwa kuwa hautupi matumaini ya kufanya vizuri kwenye michuano ya Madola.

Tunaendelea kutia shaka hasa baada ya hivi karibuni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi, kusema baadhi ya wachezaji wanaendelea na mazoezi kwenye klabu zao, lakini mazoezi ya pamoja yanategemea uwezo wa timu husika.

Tunaamini kwamba, kufanya vizuri kwa mchezaji katika michuano ya Jumuiya ya  Madola kunategemea na maandalizi bora, lakini hatuoni  nguvu ya maandalizi yake.

Tumebaki na shaka kwa kuwa mpaka sasa baadhi ya timu kama riadha, ngumi, kuogelea na paralimpiki wanaendelea kufanya mazoezi wakitokea nyumbani, badala ya wachezaji kuwa kambi ya pamoja.

BINGWA tunasema kwamba, hatuoni dalili kwa Tanzania kupata medali   katika michuano ya Jumuiya ya Madola, kwa kuwa muda uliobaki kwa wanamichezo wetu kufanya maandalizi mazuri ni mfupi.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*