googleAds

HATUACHI KITU 2020

NA WINFRIDA MTOI

SIMBA imepania kutinga robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania (ASFC) kutokana na ubora wa kikosi chake kama alivyotamba kocha wa timu hiyo, Sven Vandenbroeck.

Wekundu wa Msimbazi hao, leo wanatarajiwa kushuka dimbani kuvaana na Stand United wanaoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL), ukiwa ni mchezo wa hatua ya 16 bora wa michuano hiyo, utakaopigwa Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Simba inacheza mchezo huo ikiwa na morali ya hali ya juu baada ya kutoka kuwasha moto katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kushinda mara nne mfululizo.

Wekundu wa Msimbazi hao, walitinga hatua hiyo ya Kombe la FA baada ya kuichapa Mwadui FC mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Stand United inaujua vizuri muziki wa Simba, kwani mara ya mwisho kukutana msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara, ilichezea kichapo cha mabao mabao 3-0 Uwanja wa Taifa kabla ya kulambwa 2-0 nyumbani.

Pamoja na Stand United kubadilisha kocha na kumuajiri mbabe wa Wanamsimbazi hao katika michuano iliyopita ya ASFC, Atuga Manyundo, aliyekuwa anafundisha Mashujaa FC ya Kigoma, bado Simba ina jeuri ya kutamba.

Msimu uliopita Simba ilitolewa mapema katika mechi yake ya kwanza na Mashujaa kwa kufungwa mabao 3-2, mechi iliyochezwa Desemba mwaka juzi, Uwanja wa Taifa.

Simba kwa sasa inajivunia nyota wake hatari wanaoweza kuipa matokeo ya ushindi wakati wowote na sehemu yoyote kutokana na kuimarika kwa viwango vyao.

Wanamsimbazi hao wana nyota tishio katika kikosi hicho, wakiwamo Francis Kahata, Luis, Luis Miquissone aliyesajiliwa dirisha dogo, John Bocco, Meddie Kagere, Hassan Dilunga, Erasto Nyoni, Pasca Wawa na wengineo.

Luis kwa sasa ni mchezaji aliyeiteka shoo yote ya Simba, baada ya kuonyesha kiwango katika mechi tatu alizopewa nafasi, akionekana wazi hakuna mtu wa kuweza kumkaba kirahisi.

Kwa upande wa Stand United, ilifanikiwa kuingia hakuta ya 16 bora ya michuano hiyo kwa kuindoa Majimaji kwa mikwaju ya penalti 5-4, baada ya kumaliza dakika 90 kwa sare ya bao 1-1 kwenye dimba la Majimaji Songea.

Wakizungumzia mchezo huo, makocha wa timu zote mbili wameonekana kujiamini, kila mmoja akitamba kuibuka na ushindi.

Kocha Mkuu wa Simba Sven, alisema ana matumaini makubwa ya kushinda leo kwnai wachezaji wake wapo katika kiwango kizuri na timu inacheza kwa kuelewana.

Sven alisema kama wanavyopigana   kuhakikisha wanatetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Bara, hata michuano hiyo ni muhimu, hivyo wanahitaji kuendelea kufanya vizuri na kufika fainali kwani wamepania kutwaa kila taji la michuano wanayoshiriki.

Alisema wapinzani hawafahamu vizuri kutokana na kucheza ligi tofauti, lakini anajua jambo muhimu ni maandalizi.

“Maandalizi yetu yanalenga kushinda kila mchezo, tunakwenda kucheza na Stand United tukijua tuna jukumu la kupata pointi tatu, hivyo nitapanga kikosi cha kutupa ushindi,” alisema Sven.

Naye kocha wa Stand, Manyundo, alisema anafahamu Simba ina wachezaji wazuri wakiwamo wa kimataifa tofauti na timu yake, ila amejipanga kupambana hadi dakika ya mwisho.

“Simba ni timu kubwa na bora kutokana na rekodi zao katika Ligi Kuu, lakini wasitudharau  sisi, tuna uwezo wa  kuwaondoa kwenye michuano hii kwa sababu wachezaji wangu nimewapa mbinu zote,” alitamba Manyundo.

Michezo mingine ya michuano hiyo, itazikutanisha Mbeya City dhidi ya Namungo FC kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, Panama wataikaribisha Sahare All Stars dimba la Uhuru, wakati Ndanda FC itakuwa mwenyeji wa Kitayosa, Uwanja wa Nangwanda, Mtwara.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*